
Uelewa wetu kama Watanzania kuhusu kulinda amani ndiyo nyenzo kuu inayotuwezesha kufanya shughuli halali zinazotupatia mahitaji ya kila siku.
Amani hii inapotikiswa, madhara yake ni makubwa, kama tulivyoshuhudia hapo awali mnamo Oktoba 29, ambapo sekta binafsi ilipata hasara kubwa baada ya baadhi ya makampuni na watu binafsi uwekezaji wao kuporwa na kuchomwa moto na kupoteza kila kitu wakati wa vurugu.
Sekta binafsi ndiyo injini kuu ya ajira nchini, na bila amani, hakuna uwekezaji unaoweza kustawi. Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesisitiza kuwa Serikali inalenga kujenga uchumi wa uzalishaji na uongezaji thamani ili kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Lengo hili haliwezi kufikiwa bila ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi kama nguzo muhimu ya kukuza viwanda na kuvutia wawekezaji. Tunapaswa kulinda amani ili kuipa sekta binafsi nafasi ya kukua na kuchangia katika malengo haya ya kitaifa.
Ili kufanikisha hili, ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi ni jambo lisilo na mbadala. Ni lazima kuwepo na uaminifu ambapo raia wanajisikia salama kushirikiana na askari kulinda mali na miundombinu ya biashara mitaani.
Tanzania ni nchi ya umma ambayo imekuwa na amani tangu uhuru, na hatupaswi kuruhusu nchi yetu iyumbishwe au kuvurugwa na vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na watu wachache wasioitakia mema nchi yetu.
Tunapoelekea kipindi cha sikukuu, ni wajibu wetu sote kukataa malengo yoyote ya kuvuruga amani na badala yake kuimarisha ulinzi shirikishi. Maisha yetu na shughuli zetu za kiuchumi zinahitaji mazingira tulivu ili kila mmoja aweze kunufaika na fursa zilizopo.
Tuungane kulinda amani yetu, si kwa faida ya mtu mmoja mmoja, bali kwa ustawi wa taifa zima na sekta binafsi inayotubeba sote. Amani inaita uwekezaji, na uwekezaji unaleta maendeleo.
Tuilinde amani kwa nguvu zetu zote ili kuifanya Tanzania iwe sehemu salama na yenye ushindani katika soko la kimataifa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464