` AMANI NI JUKUMU LETU TUSHIRIKIANE NA VYOMBO VYA USALAMA KUOKOA JAMII

AMANI NI JUKUMU LETU TUSHIRIKIANE NA VYOMBO VYA USALAMA KUOKOA JAMII

Jeshi la Polisi Tanzania limethibitisha kuwa hali ya usalama nchini imeendelea kuwa shwari. Hata hivyo, ukweli ni kwamba amani ya nchi yetu inategemea zaidi uelewa wa kila Mtanzania kuhusu umuhimu wa kulinda na kuimarisha utulivu mahali alipo.

 Amani ndiyo nyenzo kuu na ya msingi inayotuwezesha sote kushiriki na kufanya shughuli halali zinazotupatia mahitaji yetu ya kila siku bila hofu.

Ili Jeshi la Polisi liweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu ya kulinda raia na mali zao, ni lazima kuwepo na ushirikiano wa karibu kati ya polisi na wananchi.

 Raia wema hawapaswi kuwaogopa au kuwakimbia askari, kwani mara nyingi wanaofanya hivyo ni wale wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu vinavyoumiza jamii.

Kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi ni hatua ya kizalendo inayosaidia kudhibiti uhalifu katika mitaa yetu.

Hata hivyo, ili kujenga imani hii, ni muhimu kwa askari wetu kuzingatia weledi kwa kutodhulumu watu kwa jeuri wala kuwashtaki raia kwa uongo. Vilevile, jamii inapaswa kuacha dhana ya kuona jeshi kama chombo kilichoingiliwa na siasa na badala yake tulichukulie kama mhimili wa ulinzi wa kila Mtanzania.

 Tukiondoa hofu na kutoaminiana, tutatengeneza mazingira ambapo mhalifu hapati nafasi ya kujificha miongoni mwetu.

Tunapoelekea kusheherekea sikukuu za mwisho wa mwaka, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi linaendelea kuimarisha ulinzi wakati wote. 

Ni wakati mwafaka kwa kila mmoja wetu kutambua thamani ya usalama katika maisha yake na kuyakataa kwa nguvu zote yale yote yenye malengo ya kuvuruga amani kipindi hiki cha sikukuu na baada ya hapo. 

Maisha yetu yanahitaji mazingira ya amani ili tuweze kushiriki ibada na kukaa na familia zetu bila bughudha yoyote.

Pia, kwa wale wanaosafiri kuelekea mikoani, ni muhimu kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuzuilika. Tukumbuke kauli mbiu inayosisitiza kuendesha kwa salama kwa ajili ya familia zinazotunsubiri.

 Tuilinde amani yetu kwa ushirikiano na kwa nguvu zetu zote ili kuifanya Tanzania iendelee kuwa mahali salama kwa kila mmoja. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464