` TCRS YAWAPA KICHEKO WANAFUNZI WA KIKE MANGU NA SHAGIHILU SEKONDARI KISHAPU

TCRS YAWAPA KICHEKO WANAFUNZI WA KIKE MANGU NA SHAGIHILU SEKONDARI KISHAPU


Na Sumai Salum – Kishapu

Shirika la Tanganyika Christian Refugee Service (TCRS) mkoani Shinyanga limeendelea kung’ara katika juhudi zake za kuwawezesha watoto wa kike, baada ya kuwagawia taulo za kike wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mangu na Shagihilu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Desemba 3, 2025.

Katika tukio hilo lililobeba matumaini na kuleta tabasamu kwa mabinti wengi, TCRS pia imetoa elimu ya kina kuhusu hedhi salama, ikieleza umuhimu wa usafi, uelewa wa mabadiliko ya miili, na kuondoa unyanyapaa uliopo katika jamii kuhusu hedhi. Elimu hiyo imelenga kuwajengea mabinti ujasiri na kuwatia moyo kutambua kuwa hedhi ni sehemu ya kawaida ya ukuaji na si jambo la kuficha wala kuogopa.

Akizungumza na wanafunzi wakati akiwasilisha mada ya Hedhi salama, Mratibu Msaidizi wa Afya ya Uzazi na Mtoto wilayani Kishapu, Rehema Jumanne, aliwatia moyo wanafunzi kutambua thamani yao na kujiamini wanapokuwa hedhi.

“Elimu ya hedhi si ya aibu; ni haki yenu. Mnapojitambua na kujua namna ya kujitunza, mnapata uhuru wa kufikia malengo yenu bila vikwazo,” amesema Rehema,akihimiza wasichana kuwa mabalozi wa usafi na afya shuleni na majumbani.

Wanafunzi wa shule hizo wameishukuru TCRS kwa msaada huo, wakisema umebadili mtazamo wao kuhusu hedhi na kuongeza ujasiri wa kuhudhuria masomo bila hofu.

Baadhi wamesema awali walikosa vifaa vya kujisitiri, jambo lililoathiri kuhudhuria masomo, lakini sasa wanahakika wa kuendelea na masomo bila kikwazo. Mmoja wa wanafunzi amesema msaada huo umewapa faraja na kuondoa changamoto walizokuwa wakikumbana nazo, huku elimu waliyopewa ikiwaongezea ujuzi, ujasiri na uwezo wa kujitunza wakati wa hedhi.

TCRS imeendelea kuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya jamii za Shinyanga, hasa katika kuwawezesha watoto wa kike kupitia elimu, afya ya uzazi, usawa wa kijinsia na uimarishaji wa fursa za elimu.

Kupitia miradi kama hii, shirika linaendelea kutoa ishara ya matumaini kwa kizazi kijacho, likiwaweka mabinti katika nafasi salama na yenye kuwatia nguvu kufikia ndoto zao.

Mratibu Msaidizi wa Afya ya Uzazi na Mtoto wilayani Kishapu Mkonai Shinyanga Rehema Jumanne,akiwasilisha mada ya hedhi salama kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mangu iliyoko Kata ya Ndoleleji na shule ya Sekondari Shagihilu zilizoko Wilayani humo Desemba 3,2025
Mwezeshaji kutoka Shirika la Tanganyika Christian Refugee Service (TCRS) Wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Venas Chunga akizungumza Desemba 3,2025 wakati wa utoaji elimu ya hedhi salama na ugawaji taulo za kike kwa wanafunzi wa Shule za Sekondari ya Mangu na Shagihilu wilayani humo
















\



































Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464