.jpg)
Katika salamu hizo zilizotolewa na
Mwenyekiti wa TBN Beda Msimbe, ameeleza maadhimisho ya Uhuru si tu siku ya
mapumziko, bali ni fursa ya kutafakari safari ya Taifa tangu kupatikana kwa
Uhuru mwaka 1961 na kuelewa wajibu wa kizazi cha sasa katika kuendeleza misingi
iliyoachwa na waasisi wa nchi.
TBN imemrejea Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere, aliyewahi kusisitiza kuwa:
“Uhuru
hauwezi kukamilika pasipo kujitegemea. Hatuwezi kuitwa huru kama tunategemea
wengine kutupatia mahitaji yetu ya kimsingi.”
Mtandao huo umesema kauli hiyo bado
ina uzito mkubwa kwa kizazi cha leo, hasa katika zama za uchumi wa kidijitali,
ambapo ubunifu, bidii na ushirikiano vina nafasi kubwa katika kuleta maendeleo.
Jukumu la Watanzania: Kulinda Amani na Kuepuka
Uchochezi
Katika ujumbe huo, TBN imesisitiza
kuwa mafanikio yaliyofikiwa na Taifa ni matokeo ya utulivu na umoja uliodumu
kwa miongo kadhaa. Mtandao huo umeonya kuwa vurugu, chuki na uchochezi vinaweza
kuyumbisha juhudi za miaka mingi za kupambana na adui ujinga, umaskini na
maradhi.
Rais mstaafu Benjamin William Mkapa
aliwahi kusema:“Amani si kitu cha
asili, tunahitaji kuilinda na kuitunza kila siku. Bila amani, hakuna maendeleo
ya kweli.”
TBN imetumia kauli hiyo kuwakumbusha
Watanzania kuwa mustakabali wa Taifa uko mikononi mwa wao wenyewe.
Kuheshimu Zama na Mwelekeo wa Uongozi
Mtandao
huo pia umeangazia umuhimu wa kuheshimu mchango wa kila awamu ya uongozi
nchini, ukimnukuu Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi aliyesema:
“Kila
utawala na zama zake. Kila kiongozi na mchango wake katika ujenzi wa Taifa
hili.”
TBN imesisitiza kuunga mkono falsafa
ya 4R inayoongozwa na Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan — Reconciliation, Resilience, Reforms, and
Rebuilding — inayolenga kuimarisha umoja wa Taifa, mageuzi na ustawi wa
wananchi.
Wito kwa Vijana na Watanzania Wote
TBN imewataka Watanzania kutumia
uhuru wa kutoa maoni kwa busara na siyo kama silaha ya kubomoa Taifa. Mtandao
huo umesisitiza kuwa,Uhuru ni wajibu,Amani ni nguzo ya maendeleo na Kujituma kufanya kazi kwa bidii ndilo deni kwa waasisi
wa nchi.
TBN inawatakia Watanzania wote
maadhimisho mema ya miaka 64 ya Uhuru,
“Tanzania Kwanza. Kazi na Utu,
Tusonge Mbele.”
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464