.jpg)
Tanzania imeendelea kung’ara kimataifa baada ya kushinda tuzo ya dunia katika sekta ya utalii kwa mwaka wa pili mfululizo, ikitambuliwa kama nchi bora zaidi duniani kwa utalii wa safari. Ushindi huo wa kihistoria unatajwa kuwa ni matunda ya uongozi bora na juhudi za Serikali katika kuhifadhi na kukuza sekta ya utalii.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, alieleza hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam walipopokelewa baada ya kurejea na tuzo tano kutoka Bahrain-Manama, nchi ya kisiwa iliyopo kati ya Saudi Arabia na Qatar, ambapo tuzo hizo zilitangazwa.
Mafanikio Yafungua Milango ya Uenyeji
Dkt. Abbas alisema kufuatia Tanzania kushinda tuzo hiyo kwa mara ya pili mfululizo, mwaka ujao wa 2026, Tanzania imepewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa tuzo hizo za dunia. Tuzo hizo mwaka jana zilifanyika Ureno na mwaka huu Bahrain.
"Hivyo mwakani, dunia, mashirika makubwa duniani na wadau wakubwa wa utalii na kampuni zote kubwa watazifuata tuzo hizo Tanzania," alisema Dkt. Abbas. Aliongeza kuwa muda wa tuzo hizo utatangazwa hapo baadaye.
Awali, Dkt. Abbas alisisitiza kuwa tuzo hii ni kubwa katika sekta ya utalii duniani, na kutambulika kwa Tanzania ni jambo kubwa sana. Aliishukuru Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na marais wengine wote waliopita, kwa kuwekeza nguvu katika uhifadhi na sekta ya utalii.
Serengeti Yashinda Hifadhi Bora Duniani
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Nchini (TTB), Ephraim Mafuru, alishukuru wadau wa sekta ya utalii kwa michango yao katika kuhakikisha Tanzania inashinda tuzo hiyo. Alisisitiza kuwa ushindi huo unathibitisha kuwa dunia imetambua ubora wa vivutio vya utalii vya Tanzania.
Mafuru alipongeza hususani Hifadhi ya Serengeti ambayo ilishinda tuzo ya Hifadhi Bora Duniani. Alisema Tanzania ina mafanikio makubwa katika uhifadhi, kwa sababu sio tu nchi yenye vivutio vya wanyamapori bali maeneo mengi ya kipekee, ikiwemo mapori ya akiba na misitu.
Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuboresha miundombinu ya utalii, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara katika maeneo ya hifadhi.
Wito wa Amani na Utulivu
Mafanikio haya yanatumika kama mfano wa jinsi matunda ya uongozi bora, utulivu, na amani yanavyoweza kukuza Taifa kiuchumi. Watanzania wanahimizwa kuendelea kuwa wapole, kujenga Taifa, na kuacha tabia ya kujutia kwa kufuata uchochezi, kwani maendeleo haya yanahitaji utulivu wa kudumu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464