` RAIS SAMIA: TUMEJIPANGA, TUTAILINDA NCHI HII KWA NGUVU ZOTE

RAIS SAMIA: TUMEJIPANGA, TUTAILINDA NCHI HII KWA NGUVU ZOTE

 Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa serikali yake itaendelea kulinda mipaka, usalama wa raia na mali zao kwa nguvu zote, akibainisha kuwa vurugu za hivi karibuni zilizoripotiwa wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, zilidhamiria kuangusha Dola na hazikuwa na asili ya Kitanzania.


Akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam leo, Rais Samia alihoji ukosoaji wa matumizi ya nguvu za dola, akisema: "Tunaapa kuilinda nchi hii na mipaka yake, kulinda usalama wa raia na mali zao... Tunapoambiwa kwamba tulitumia nguvu kubwa sana kwenye tukio lile, nguvu ndogo ilikuwa ni ipi? Ilikuwa tuwangalie waandamanaji waliojiandaa kufanya mapinduzi mpaka wafanikiwe, hapo kutakuwa na Dola?"

Tupo Tayari Kuwapokea Waliojipanga

Rais Samia alifichua mipango ya uhamasishaji wa vurugu inayoratibiwa na waandaaji wa nje, huku akisisitiza kuwa serikali imejiandaa wakati wote.

"Nilimsikia mmoja kati ya waandaaji wa nje anasema tarehe 9 (siku waliyopanga maandamano) iahirishwe isubiriwe siku ya Krismasi sababu sasa hivi tumejipanga... nataka niwaambie wakati wowote wakija tumejipanga," alionya Rais Samia.

Alieleza kuwa vurugu za Oktoba 29 na 30 ni 'mradi mpana sana' na tukio la kutengenezwa ambapo vijana walihamasishwa kufanya kama yaliyotokea Madagascar bila hata kujua wanachotaka.

"Vurugu za tarehe 29 na 30 si desturi wala utamaduni wa Watanzania... inatia uchungu kuona wachache walioratibu fujo zile wakitaka Watanzania wenzao wawe kafara kwa malengo yao ya kisiasa yaliyojaa ubinafsi," alieleza.

 Serikali Haitaendeshwa na Madhehebu ya Dini

Katika hotuba hiyo, Rais Samia alitoa msimamo mkali kwa taasisi za dini, akisisitiza kuwa hakuna dhehebu lolote lenye mamlaka ya kuiendesha serikali au kutoa matamko yanayo 'override' madhehebu mengine au Katiba.

"Kikatiba na sheria za nchi hakuna madhehebu hata moja ya dini yoyote imepewa uwezo... Hatutaendeshwa na madhehebu yoyote ya dini," alisema.

Aliongeza kuwa Watanzania wana dini, lakini nchi haina dini, na hakuna kitabu chochote cha dini kinachofundisha kuvuruga amani ya nchi. Aliwataka viongozi wa dini kutovaa majoho yao kutengeneza utashi binafsi na chuki dhidi ya viongozi.

Vijana Kukosa Uzalendo Kumechangia, Wizara Kuundwa

Kuhusu vijana waliohusika kwenye vurugu, Rais Samia alikiri kwamba matukio hayo yametokana na ukosefu wa elimu ya uzalendo, na kutokana na kujifunza hilo, Wizara nzima ya Vijana imeundwa ili kushughulika na masuala yao kwa upeo mpana na kuwajengea uzalendo.

Wazee Waunga Mkono 

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dar es Salaam, Salum Matimbwa, alisifu hatua zilizochukuliwa na Rais Samia baada ya vurugu, akisema zimedhihirisha uimara wake na uongozi unaoelekezwa na falsafa yake ya 4R.

Matimbwa alibainisha kuwa falsafa hiyo ya 4R inajumuisha: Mageuzi (Reform), Maridhiano (Reconciliation), Ustahimilivu (Resilience) na Kujenga Upya (Rebuilding), hatua ambazo zimepelekea kuundwa kwa Tume ya Uchunguzi na kutoa msamaha kwa vijana waliofuata mkumbo.

Pia, alipongeza uamuzi wa kuanzisha Wizara ya Vijana na ahadi ya bima ya afya bure kwa wazee.
"Sisi wazee siku zote tutakuwa bega kwa bega na wewe kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa ilivyotulia," alihitimisha Matimbwa.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464