` PROF. SHEMDOE AMTAKA MKANDARASI ANAYEJENGA MAHAKAMA YA WILAYA YA LUSHOTO KUWAPA KAZI WAZAWA

PROF. SHEMDOE AMTAKA MKANDARASI ANAYEJENGA MAHAKAMA YA WILAYA YA LUSHOTO KUWAPA KAZI WAZAWA

 

Na James Mwanamyoto - Lushoto

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amemuelekeza Mkandarasi Namis Cooperate Limited aliyepewa kandarasi ya Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto, kuwapatia vijana wazawa na akina mama kazi zote ambazo hazihitaji utaalam ili kutengeneza ajira zitakazowapatia kipato ambacho kitainua uchumi wao.

Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo leo  Disemba 31, 2025 wilayani Lushoto, wakati wa hafla ya kupokea eneo la Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto iliyohudhuriwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel, viongozi wa mkoa na wilaya,  watumishi wa Mahakama  na wananchi wa Lushoto.

Prof. Shemdoe amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa kiasi cha Shilingi Bilioni 4.272 kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama hiyo  ambapo ujenzi wake utawapatia kipato vijana watakaopewa kazi kwenye ujenzi wa jengo hilo.

“Mkandarasi ninakuomba huku nikikuelekeza kwamba, kazi zote ambazo hazihitaji expert wapewe vijana wetu wa hapa Lushoto ili tuweze kutengeneza ajira kwa vijana wetu wa hapa Lushoto,” Prof. Shemdoe amesisitiza.

Sanjari na hilo, Prof. amemtaka mkandarasi huyo kununua bidhaa za ujenzi zinazopatikana wilayani Lushoto ili kuongeza mzunguko wa fedha kwa wakazi wa wilaya hiyo ya Lushoto.

Pia, Prof. Shemdoe amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kuhakikisha anavikopesha fedha vikundi vya akina mama kupitia mikopo ya asilimia 10, ili vijishughulishe na biashara ya kuwauzia chakula vijana watakaoajiriwa kwenye mradi huo wa Ujenzi wa Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Lushoto.

Aidha, Prof. Shemdoe ameushukuru ushirika wa kupanda kahawa Lushoto (coffee growers association) kwa uzalendo wao kwa kutoa bure eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 6,269 kwa ajili ya Ujenzi wa jengo hilo la Mahakama. 

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kuwa mkataba wa ujenzi wa Mahakama hiyo uliosaniwa leo hautakuwa na nyongeza ya muda wa mkataba wala nyongeza ya gharama, hivyo watasimamia ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati kwani wananchi wanashauku ya kuhudumiwa katika jengo jipya la Mahakama ya Wilaya. 

Mmoja wa wakazi wa Kata ya Magamba Wilayani Lushoto Bw. Salimu Omary amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Lushoto ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe kwa kumuelekeza mkandarasi kuwapatia kazi vijana wazawa ili  kupata kipato kitakachoendesha maisha yao.

Naye mkazi mwingine wa Wilaya ya Lushoto Bw. Shaban Adam Mbwana amesema yeye binafsi atachangamkia fursa hiyo ya ajira kwenye mradi huo wa ujenzi wa jengo la Mahakama kwani ana watoto ambao wanahitaji kulipiwa ada shuleni hivyo atakuwa mnufaika wa mradi huo.

Kiasi cha Shilingi Bilioni 4,271,942,834.98 kitatumika kukamilisha mradi huo wa Ujenzi  wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto, ujenzi ambao unatarajiwa kutoa  ajira kwa vijana, akina mama lishe na wafanyabiashara wa wilayani Lushoto.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464