
Tume ya Kuchunguza Matukio ya uvunjifu wa Amani yaliyotokea Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 imetangaza rasmi kuanza kutekeleza majukumu yake makuu, ikiwemo uchunguzi wa kina wa malalamiko yaliyotolewa na wananchi.
Uchunguzi huu unalenga kutoa mwanga juu ya matukio yaliyotokea, hususan vurugu za Oktoba 29, na unatazamiwa kuwa hatua muhimu sana katika harakati za kujenga maridhiano na uponyaji wa kitaifa nchini Tanzania.
Mwenyekiti wa Tume, Jaji Othman alisisitiza kwamba Tume imepewa jukumu la kisheria la kuchunguza kwa kina kila taarifa, ushahidi, maoni, na mapendekezo yatakayosaidia kujua ukweli. Kusudi kubwa ni kuhakikisha haki inatendeka na kuimarisha amani nchini .
Mtazamo wa Wadau:
Kuanza kwa kazi hiyo kumeitikiwa vyema na wadau mbalimbali. Viongozi wa dini wameelezea Tume hiyo kama "daraja la kuunganisha" linalotoa fursa kwa wananchi kuondoa mizigo mioyoni mwao.
"Kwa sisi kama viongozi wa dini, ushiriki wa kila mmoja katika kutoa ukweli ni sawa na kuweka msingi thabiti wa maridhiano. Ukweli ndio unaoweza kuponya majeraha ya jamii" .
Wataalamu wa sheria na siasa wanasisitiza kwamba michango kutoka kwa wananchi ni muhimu ili Tume ifanye kazi kwa uhalali na kujiamini.
Wananchi nao wanaona hatua hii kama fursa ya kipekee ya kuwasilisha malalamiko yao, matukio ambayo yamekuwa yakiwaumiza, na kusaidia kufanya tume kuwa chombo cha kweli cha jamii.
Ushiriki huu, kwa mujibu wa wataalamu, ndio utakaofanya ripoti ya Tume iweze kukubalika na kutekelezwa, hivyo kufungua njia ya kweli kuelekea maridhiano ya kitaifa.
Tume katika taarifa yake inatoa wito maalum kwa kila Mtanzania anayeipenda nchi na anayejali amani, hasa wale walioshuhudia au wana taarifa zinazohusu matukio hayo, kujitokeza na kuwasilisha taarifa zao kwa ukweli na uwazi.
"Huu si wakati wa woga, bali ni wakati wa uzalendo wa kusaidia Tume kufikia ukweli kwa ajili ya mustakabali wa nchi yetu."
Taarifa zinazopokelewa ni pamoja na nyaraka za maandishi, picha (mnato au mchoro) na video (kama kanda ya sauti au rekodi) zinazohusu matukio ya uvunjifu wa amani, vitendo vya kihalifu, vurugu, au ukiukwaji wa haki uliofanywa na wadau mbalimbali.
Njia za Kuwasilisha Taarifa:
Ili kuhakikisha kila mwananchi anapata fursa ya kusaidia, Tume imetoa njia kadhaa za kuwasilisha ushahidi na mawasiliano. Taarifa za kimaandishi, nyaraka, au ushahidi unaowasilishwa kwa mkono unaweza kupelekwa kupitia Sanduku la Barua la Tume: Tume ya Uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu oktoiba 2025, S.L.P 471, Dar es Salaam.
Kwa mawasiliano ya kielektroniki, wananchi wanaweza kutumia barua pepe kwenye anwani ya tovuti tume.uchunguzi@go.tz au barua pepe ya tume.uchunguzi@gmail.com.
Aidha, Tume itapokea Ujumbe Mfupi wa Simu (SMS) au WhatsApp kupitia namba zifuatazo: 0743 040890 au 0737 305449. Mawasiliano pia yanawezekana kupitia mitandao ya kijamii, ambapo wananchi wanaweza kutuma taarifa kwa Tume kupitia tume_u-chunguzi kwenye majukwaa ya Instagram na X (Twitter).
Tume inawaomba Watanzania kutumia fursa hii muhimu ya kihistoria kusaidia kazi ya uchunguzi ili Tume iweze kukamilisha majukumu yake kwa wakati na kwa ufanisi, na hatimaye kusaidia kuleta suluhisho la kudumu kwa ajili ya umoja na maridhiano nchini.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464