
Amani imeshinda. Katika nchi yetu, sauti ya utulivu imezidi kelele za chuki, propaganda na miito ya uasi, kufuatia wito ulioendelea kutolewa na wananchi na makundi mbalimbali ya kijamii nchini, ikiwemo wanasiasa.
Wananchi hao wanataka ushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa maridhiano ulioasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ili kuondoa tofauti, kero na changamoto zilizopo nchini kupitia mazungumzo.
Basil Kayombo, mkazi wa Dar es Salaam, ameeleza bayana kuwa vurugu, migomo na maandamano hayajawahi kuwa chanzo cha kuondoa matatizo na tofauti za kijamii na kisiasa kote duniani.
"Ombi langu kwa wananchi tuendelee kuombea amani, haki na watoto wetu pia waelewe yale wanayoshauriwa. Kwa wanaohamasisha maandamano niwaombe waendelee kuzungumza na kuishauri serikali nini cha kufanya. Njia nzuri ya kutatua matatizo ni kuzungumza na vurugu na migomo haisaidii kitu," amesema Kayombo.
Kwa upande wake, Tumaini Anzali, Mkazi wa Ubungo jijini Dar es Salaam, amemshukuru Mungu kwa kuendelea kuilinda amani ya Tanzania kiasi cha kuwaruhusu wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi, huku akihimiza vijana pia kudumisha amani kwa mustakabali wa ustawi na maendeleo yao. Ujumbe huo unaungwa mkono na falsafa kwamba amani haiwezi kudumu bila haki, lakini haki haiwezi kupatikana kwa ghasia.
Wakati wananchi wakishikilia msimamo wa amani, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, amewataka wananchi wa mkoa huo kuendeleza utamaduni wa kukataa maandamano na matukio yoyote yenye viashiria vya uvunjifu wa amani.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za biashara katika Soko la Kilombero jijini Arusha, Makalla ameahidi kuwa Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama itaendelea kuhakikisha amani na usalama vinadumishwa.
“Dunia imeona, na Watanzania wameithibitishia dunia kwamba wakiamua kulinda amani wanailinda. Watanzania wanapenda amani na hawajazoea maandamano au uvunjifu wa amani. Wale waliotaka vurugu leo wamejifungia na wana maumivu kwa kuwa hawakufanikiwa,” amesema Makalla, akionyesha kuridhishwa na utamaduni wa amani wa Watanzania.
Aidha, kiongozi huyo amewahimiza wananchi kujikita zaidi katika shughuli za kiuchumi na kijamii, huku akionya kuwa vyombo vya ulinzi na usalama viko imara kukabiliana na watu wote watakaopanga kufanya vitendo vya uhalifu au kuchochea uvunjifu wa amani katika Mkoa wa Arusha.
Kwa ujumla, wito mkuu unaendelea kuwa, tunapodai haki, amani ikumbukwe kama chombo cha mazungumzo, kwani vurugu ni urithi wa maumivu, na amani ni msingi wa maendeleo.