Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga na Mwenyekiti wa kamati ya lishe wilayani humo, Mhe. Peter N. Masindi akizungumza kwenye kikao cha kujadili taarifa za utekelezaji wa Mkataba wa Lishe ngazi ya Wilaya, Kata na Vijiji kwa kipindi cha Julai–Septemba 2025, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Disemba 17,10125
Na Sumai Salum – Kishapu
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga na Mwenyekiti wa kamati ya lishe wilayani humo, Mhe. Peter N. Masindi, amewataka wanaume kushiriki kikamilifu katika elimu ya lishe ili kujenga familia bora, zenye afya na ustawi endelevu, akisisitiza kuwa suala la lishe si la wanawake pekee bali ni jukumu la wazazi wote.
Masindi ametoa wito huo Disemba 17, 2025, wakati wa kikao cha kujadili taarifa za utekelezaji wa Mkataba wa Lishe ngazi ya Wilaya, Kata na Vijiji kwa kipindi cha Julai–Septemba 2025, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Masindi amewakumbusha Watendaji wa Kata kuwa wao ni wasimamizi wa karibu wa sera na mikakati ya lishe katika jamii, hivyo wanapaswa kuweka mkazo katika kusimamia utekelezaji wa afua zote za lishe kwa vitendo.
“Wajibu wetu kama wasimamizi wa sheria na kama wazazi ni kuhakikisha watoto wetu wanakuwa na afya bora na imara pamoja na lishe bora. Hapo ndipo tunajenga kizazi salama kitakachoweza kuendesha familia, jamii na Taifa kwa nidhamu na umoja,” amesisitiza Mhe. Masindi.
Ameongeza kuwa lishe bora kwa watoto, hasa walio chini ya miaka mitano, na kwa wanawake wajawazito si jambo la hiari bali ni uwekezaji wa moja kwa moja katika afya ya kizazi cha sasa na kijacho. Mtoto anayepata lishe sahihi tangu tumboni na katika miaka ya mwanzo ya ukuaji huwa na uwezo mzuri wa kimwili, kiakili na kielimu, hali inayosaidia kujenga Taifa lenye nguvu kazi yenye tija,” amesema.
“Wanawake wajawazito wanapopata lishe bora hulinda maisha yao na ya watoto wanaowabeba, na hupunguza hatari za vifo vya mama na mtoto pamoja na matatizo ya kiafya yanayoweza kuzuilika. Hivyo ni wajibu wa familia, jamii na viongozi wote, hususani Watendaji wa Kata na Vijiji, kusimamia na kuhimiza utekelezaji wa afua za lishe kwa umakini na uwajibikaji,” amesisitiza
Aidha, amewahimiza viongozi hao kuhakikisha elimu ya lishe inawafikia wananchi wote, ikijumusiha hasa kundi la wanaume ambao ndio watoaji wa fedha za matumizi majumbani, ili kuondoa dhana potofu kuwa masuala ya lishe ni jukumu la mama pekee.
"Naendelea kuhimiza kuhusu lishe mashuleni hakikisheni watoto wetu watakapofungua shule suala la kupata chakula chenye mchanganyiko wa kitaalamu kinapatikana hiyo itawasaidia kuwa shapu katika masomo yao na pia mkumbuke kufanya maadhimisho ya siku ya lishe kikamilifu kwenye kila kijiji (SALIKI)" ameongeza Mkuu huyo wa Wilaya
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Joseph Bahati, amesema bado kuna wajibu mkubwa kwa Halmashauri na viongozi wa ngazi zote kusimamia masuala ya lishe mashuleni na majumbani, hususan kwa watoto walio chini ya miaka mitano na wanawake wajawazito.
“Tunalo jukumu la kuhakikisha watoto wetu wanapata lishe sahihi tangu wakiwa wadogo, huku akina mama wajawazito wakipata mlo kamili ili kuzuia udumavu na changamoto nyingine za kiafya,” amesema Dkt. Bahati.
Naye Afisa Lishe wa Wilaya ya Kishapu Furaha Kaburwa, akizungumza wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa afua za lishe kupitia Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, amesema Wilaya imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha lishe ikiwemo utoaji wa elimu ya lishe ngazi ya jamii, ufuatiliaji wa watoto walio hatarini kupata utapiamlo pamoja na kuhimiza matumizi ya vyakula vyenye virutubisho.
“Ushirikiano wa Watendaji wa Kata, viongozi wa vijiji na wadau wa maendeleo ni muhimu sana ili kuhakikisha jitihada hizi zinaleta matokeo chanya kwa jamii,” amesema Afisa Lishe huyo.
Wakati huo huo, Meneja Mradi wa Shirika la REDESO Wilaya ya Kishapu, Bw. Charles Buregeya, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za shirika hilo, amesema REDESO limefanikiwa kusaidia jamii kujiinua kiuchumi huku ikipata lishe bora kupitia miradi ya kilimo cha bustani na ufugaji wa kuku chotara.
Amesema miradi hiyo imechangia kuongeza upatikanaji wa chakula chenye lishe pamoja na kipato kwa kaya, hali inayosaidia kuboresha afya ya familia na kupunguza changamoto za utapiamlo katika Wilaya ya Kishapu.
Sambamba na hayo shirika la WorldVision pia linatekeleza afua mbali mbali za lishe katika kata za Ngofila,Lagana na Mwamashele kwa kutoa elimu ya lishe kupitia maafisa lishe,watoa huduma za afya ,wahudumu wa afya ngazi ya jamii,kuunda vikundi malezi kwa lengo la kujifunza na kupata elimu ya afya na lishe na kitoa vyakula tiba vya matibabu ya utapiamlo mkali.