` RC MHITA ATOA MAELEKEZO YA SERIKALI KIKAO NA MADIWANI SHYDC

RC MHITA ATOA MAELEKEZO YA SERIKALI KIKAO NA MADIWANI SHYDC

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, amefanya kikao na Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na Wakuu wa Idara na kutoa maelekezo ya serikali katika kuhudumia wananchi.

Amefanya kikao hicho leo Desemba 17, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo.
Akitoa maelekezo ya serikali kwa madiwani, amesema kwamba wanapaswa wafanye mikutano ya hadhara ya kusikiliza kero na mahitaji ya wananchi, kuwa vipaumbele vyao ni vipi ili wapate kutekelezewa miradi hiyo.

“Madiwani wafanyeni mikutano ya hadhara, msikilize kero za wananchi na changamoto ambazo zinawakabili kisha muipelekee serikali ili izitatue haraka, sababu nyie ndiyo wawakilishi wenu, na Serikali hii chini ya Rais Samia Suluhu Hassan hatuna shida ya fedha ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” amesema Mhita.
Aidha, amewataka Madiwani hao kama wanapata kikwazo chochote kwenye Kata juu ya utekelezwaji wa miradi ya maendeleo kwamba wampatie taarifa ili ashungulikie na kikwazo hicho, huku akitoa agizo kuwa madiwani wawe wanapewa taarifa ya fedha kutoka Serikali kuu, na miradi ambayo inakwenda kutekelezwa kwenye kata zao.

Ametoa pia maagizo, kwa Menejiment ya Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, kwamba kero hizo zinapowasilishwa na madiwani wawe wanazitatua haraka, pamoja na kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi na kutimia lugha nzuri.
Ameagiza pia usimamizi wa miradi ya maendeleo, na kufanyike ukaguzi wa miradi hiyo na iwe yenye ubora, na kwamba hivi karibuni atafanya ziara kwenye sekta zote kukagua miradi ya maendeleo na ataanza kwenye sekta ya elimu.

Katika hatua nyingine, ameagiza suala la kuziba mianya ya upotevu wa mapato, pamoja na kuibua nyanzo vipya ya mapato.
“natoa siku 30 Malori ambayo yanapaki pale Tinde na kuhatarisha usalama, yasiwepo bali yatengeeni eneo na mkusanye mapato, na pia boresheni mnada wa Tinde na tujue mapato yake,”anasema Mhita.

Pamoja na mambo mengine Mkuu huyo wa Mkoa, amesisitiza suala la utunzaji wa chakula, pamoja na wananchi kutumia mvua zinazonyesha kulima mazao yanayostahimili ukame.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Seth Msangwa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Dk.Kalekwa Kasanga, wamesema maelekezo yote ambayo yametolewa na Mkuu huyo wa Mkoa watayafanyia kazi.

TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza kwenye kikao na Madiwani.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Ibrahimu Makana akizungumza kwenye kikao hicho.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza kwenye kikao hicho.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Seth Msangwa akizungumza kwenye kikao hicho
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dk.Kalekwa Kasanga akizungumza kwenye kikao hicho.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dk.Kalekwa Kasanga akisikiliza maelekezo ya Mkuu wa Mkoa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Seth Msangwa, (kushoto) akiwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Joseph Buyugu (kulia) na Mkurugenzi wa Halmashauri Dk.Kalekwa Kasanga kwenye kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga wakisikiliza Nasaha na maelekezo ya Serikali.
Mbunge wa Jimbo Itwangi Azza Hillal Hamad akiwa kwenye kikao hicho.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464