Boma la Zahanati Kiijiji cha Buyubi.
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
WANANCHI wa Kijiji cha Buyubi Kata ya Puni wilayani Shinyanga, wamepaza sauti kwa diwani wao Mhandisi Jumanne Rajabu, ambaye ndiyo awamu yake ya kwanza kwenye uongozi, kuikamilisha Zahanati ya Kijiji hicho ambayo imechukua miaka 18 kushindwa kukamilika kujengwa.
Wamepaza kilio hicho jana kwenye mkutano wa hadhara wa diwani wao wa kuwashukuru kumchagua Oktoba 29, pamoja na kusikiliza vipaumbele vyao vya miradi ya maendeleo.
Wananchi hao wamesema walijitolea nguvu kazi, kuanzisha ujenzi wa Zahanati hiyo tangu mwaka 2007 na kuishifikisha hatua ya renta, lakini hadi sasa haijakamilika kujengwa, na tayari kuta zimeanza kupasuka na nyingine kuanguka kutokana na kusimama kwa muda mrefu bila ya kuendelezwa.
Mmoja wa wananchi hao Hamisa Mjanahel, amesema wanasikitika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika vijiji jirani, na wakati boma la Zahanati lipo kijijini kwao usawa wa renta, na hivyo kumuomba diwani awasaidie kuikamilisha ili wapate huduma jirani na makazi yao.
“Kilio chetu kikubwa ni zahanati. Juzi binti yangu alipata uchungu saa saba usiku, tukahangaika kutafuta bodaboda hadi saa tisa ndipo tukampeleka zahanati ya Kijiji cha Kigwang’ona. alijifungua kwa bahati, lakini mtoto alikuwa amechoka sana,” amesema Hamisa.
Mwananchi mwingine Magreth Masalu, amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, asikie kilio cha wanawake wa kijiji cha Buyubi, kuwasaidia ukamilishaji wa Zahanati hiyo, kwamba wamekuwa wakiteseka kujifungua, na wakienda Zahanati za vijiji jirani, wanadai na zenyewe zina watumishi wawili tu, nesi na daktari wake.
Naye Diwani wa Kata ya Puni Mhandisi Jumanne Rajabu, amesema boma la Zahanati hiyo limekuwa kero kwa wananchi, kwa kuchukua muda mrefu bila kukamilika, na kwamba atakwenda kuipigia kelele kwenye Halmashauri ili itengewe bajeti ya kuikamilisha na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Amesema yeye ndiyo awamu yake ya kwanza ameingia kwenye uongozi kuwa Diwani Kata ya Puni, na kuwatoa hofu wananchi kwamba, atawawakilisha vizuri pamoja na kusemea matatizo yao na kutatuliwa, sababu Rais Samia ni Mama mwenye huruma, msikivu na mwenye kujali wananchi wake, hivyo boma la Zahanati hiyo lina kwenda kuwa historia kupitia uongozi wake.
Ametaja pia vipuambele vingine ambavyo zilitajwa na wananchi vikiwamo vya upatikanaji wa huduma ya maji, umeme ngazi ya vitongoji, miundombinu ya barabara na vivuko vya wanafunzi, kwamba navyo atavifanyia kazi ili vipate kutatuliwa.
Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, akizungumza kwenye kikao na Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, aliwaagiza Madiwani hao, kufanya mikutano ya hadhara ya kusikilizao kero na vipaumbele vya wananchi na kuviwasilisha halmashauri kwa utekelezaji, akisisitiza kuwa katika utawala wa Rais Samia hakuna uhaba wa fedha za miradi ya maendeleo.
TAZAMA PICHA 👇👇
Mwananchi wa Kijiji cha Buyubi Hamisa Mjanaheli akipaza kero ya Zahanati.
Mwananchi Magreth Masalu akipaza sauti ya Zahanati na kutoa vipaumbele.
Wananchi wakiendelea kutoa kero zao kwa diwani na vipaumbele.
Diwani wa Kata ya Puni Mhandisi Jumanne Rajabu akizungumza na wananchi wake wa Kijiji cha Buyubi na kuwahakikishia kero na vipaumbele vyao vitafanyiwa kazi.
Diwani wa Kata ya Puni Mhandisi Jumanne Rajabu akizungumza na wananchi wake wa Kijiji cha Buyubi na kuwahakikishia kero na vipaumbele vyao vitafanyiwa kazi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464