.jpg)
Katika kuelekea mwishoni mwa mwaka 2025, mjadala mpana umeibuka nchini Tanzania kuhusu uhusiano uliopo kati ya amani ya nchi na usimamizi wa rasilimali kwa faida ya vizazi vijavyo.
Mwandishi wa Habari wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Jackson Mwanuzi, amewahimiza Watanzania kuheshimu kauli za viongozi zinazosisitiza ulinzi wa rasilimali za taifa.
Akizungumza katika kipindi cha Mada Kuu, Mwanuzi alibainisha kuwa mataifa ya Afrika yanapaswa kujitafakari juu ya matumizi sahihi ya rasilimali watu, hususan vijana, ambao ndio injini kuu ya maendeleo barani humu.
Hali hii inaungwa mkono na Joshua Mahenge, mkazi wa Dodoma, anayeeleza kuwa nchi yenye amani inatoa fursa pana ya kutekeleza mipango ya maendeleo na kuhakikisha kuwa ushindi wa wananchi unatafsiriwa katika ujenzi wa jamii yenye usawa.
Mahenge anasisitiza kuwa utulivu unajenga taifa thabiti lenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kijamii. Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba Chacha, anatahadharisha kuwa maendeleo hayo hayawezi kufikiwa bila uadilifu.
Dkt. Rioba anafafanua kuwa uadilifu ni tabia ya kufanya yaliyo sahihi kwa uaminifu na haki, bila kushawishiwa na rushwa au maslahi binafsi, na kuwataka vijana kuwa na shauku ya kuliunganisha bara la Afrika ili kupata nguvu ya pamoja katika maamuzi.
Mjadala huu unakuja wakati ambapo uzoefu wa kihistoria unaonyesha kuwa sera za kulinda rasilimali mara nyingi hukumbana na upinzani. Balozi mstaafu, Dkt.
Mangachi Msuya, anabainisha kuwa sera za Hayati Mwalimu Nyerere zilipingwa na mataifa ya Magharibi kwa sababu zililenga kuzuia unyonyaji wa rasilimali za Tanzania.
Kwa mujibu wa Dkt. Msuya, ili Afrika inufaike kikamilifu, ni lazima rasilimali zitumike kwa kuzingatia maslahi ya Waafrika wenyewe, jambo linalohitaji utulivu wa ndani na mshikamano wa kitaifa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464