Na Johnson James, SHINYANGA
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita amewataka Wakuu wa Divisheni za Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na Maafisa Ugani kuendelea kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu umuhimu wa chanjo na utambuzi wa mifugo ili kuongeza usalama na thamani ya mifugo yao.
Mhe. Mhita alitoa wito huo Disemba 12, 2025 wakati wa hafla ya kukabidhi pikipiki 14 kwa Maafisa Ugani wa Mifugo kutoka halmashauri zote sita za mkoa, tukio lililofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kada za kilimo na mifugo.
Pikipiki hizo zenye thamani ya milioni 44 zimetolewa na Wizara ya Mifugo ili kurahisisha ufuatiliaji na utoaji wa huduma kwa wafugaji.
Kupitia ugawaji huo, Manispaa ya Shinyanga na Kahama zimepokea pikipiki moja moja, huku Halmashauri za Shinyanga, Ushetu, Msalala na Kishapu zikipewa tatu kila moja.
RC Mhita amewataka Maafisa Ugani kuhakikisha pikipiki hizo zinatumika kikamilifu kuhamasisha wafugaji kuchanja mifugo na kushiriki zoezi la utambuzi ili kudhibiti magonjwa na kuongeza tija kwa wafugaji.
Aidha, amezitaka Halmashauri kupitia Wakurugenzi kutenga fedha za ndani kuendeleza zoezi hilo kwa kushirikiana na Sekta Binafsi na Vyama vya Ushirika, ili kuhakikisha linafikia wafugaji wote kwa wakati.
Katibu Tawala wa Mkoa, CP Salum Hamduni, amesema pikipiki hizo zitatumika kuongeza kasi ya huduma ya chanjo na utambuzi wa mifugo katika maeneo ambayo awali yalikuwa hayafikiki kwa urahisi.
Naye Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Uchumi na Uzalishaji, Bw. Raphael Nyanda, amesema mkoa una zaidi ya mifugo milioni 4.1, hivyo pikipiki hizo zitasaidia kutekeleza maagizo ya Rais Samia aliyoyatoa wakati wa uzinduzi rasmi wa zoezi hilo Mei 18, 2025 mkoani Simiyu.
Wakuu wa Divisheni za Kilimo wakiongozwa na Deus Antony ambaye ni Mkuu wa Divisheni kutoka halmashauri ya Ushetu amesema wameishukuru Serikali kwa kuwapatia vitendea kazi vitakavyowawezesha kuwafikia wafugaji na kuongeza ufanisi wa chanjo na utambuzi wa mifugo, zoezi linalotarajiwa kudumu hadi mwaka 2029.



