Na Marco Maduhu, SHINYANGA
MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali (NGOs) wilayani Shinyanga, yamelalamikia baadhi ya vifungu vya sheria za kodi, kuyalazimisha kulipa kodi kama makampuni ya kibiashara na wakati miradi yao inatoa huduma kwa jamii.
Hayo yamebainishwa leo Desemba 12,2025 na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali (NaCoNGo) wilaya ya Shinyanga Lucas Maganga, wakati akisoma risala kwenye kikao cha Robo mwaka cha mashirika hayo kuanzia Septemba –Desemba mwaka huu.
Amesema richa ya serikali kuwatatulia changamoto mbalimbali ambazo zilikuwa zikiwakabili hapo awali, bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa na kuomba zitatuliwe ikiwamo ya utozwaji kodi kubwa kama makampuni ya kibiashara, na ugumu na urasimu wa kupata Charitable Status kutoka TRA.
Aidha, ametoa mapendekezo kwamba kufanyike mapitio ya pamoja ya miongozo ya TRA ili kutofautisha miradi ya kijamii isiyo ya kibiashara na shughuli zenye mapato, TRA kuanzisha dawati maalum la kushughulikia masuala ya mashirika ngazi za wilaya na mkoa ili kurahisha kufuatilia maombi ya misamaha ya kodi.
Mapendekezo mengine ni ushirikishwaji wa wadau wa NGOs wakati wa marekebisho ya sera na sharia za kodi ili kuleta uelewa wa pamoja na kupunguza gharama zisizo za lazima, kupunguza ngazi za idhini na kuweka utaratibu wa “one stop center” ili kurahisisha mchakato wa kupata “Charitable Status.”
“Tunatambua kwa dhati mchango mkubwa wa serikali katika kuboresha mazingira ya mashirika yasiyo ya kiserikali kufanya kazi kwa ufanisi, tunaamini kuwa changamoto hizi zikishughulikiwa, tutajenga mfumo imara Zaidi wa ushirikiano kati ya Serikali na NGOs na hivyo kuongeza tija katika kuwaletea wananchi maendeleo,”amesema Lucas.
Aidha, ameipongeza serikali kwa kutekeleza baadhi ya Changamoto ambazo zilikuwa zikiwakabili hapo awali, ikiwamo upatikanaji wa vibali vya utekelezaji wa miradi kwa wakati tofauti na hapo awali ambapo kulikuwa na urasmu, pamoja na utekelezaji mzuri wa miradi,
Pia, ameyapongeza mashirika yote ambayo yameendelea kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na kujitolea katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki katika maeneo ya afya, elimu, maji, mazingira, uchumi wa jamii, ulinzi wa mtoto na makundi maalum.
Kwa upande wake Mgeni Rasmi Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, ameyapongeza mashirika hayo kwa kuendelea kufanya kazi za kuhudumia jamii, na kwamba changamoto ambazo wameziwasilisha zitafanyiwa kazi, huku akishauri waanzishe “Official Communication katika eneo la Sheria”.
Aidha, ameyataka mashirika hayo yaongeze juhudi katika kuhuisha mipango kazi ili iwe ya uhakika na yenye tija, kupanua wigo wa maeneo ya kuhudumia wananchi, kuongeza juhudi za utendaji kazi, na kwamba wingi wa mashirika wilayani humo yaendane na tija, na mashirika yasiyo na tija yafutwe.
Katika hatua nyingine, amewashauri mashirika hayo kuanzia mwakani 2026, yabuni kutafuta miradi ya kudumisha Amani, usalama, utengamo na ushauri kwa vijana, na kwamba maeneo hayo yana ufadhiri mkubwa, miradi ambayo imekuwa ikipewa kipaumbele, na hata Rais Samia Suluhu Hassan ameanzisha Wizara ya Vijana.
Amesema, serikali itaendelea kushirikiana na mashirika sababu yamekuwa yakifanya kazi mbadala wa serikali katika kuwahudumia wananchi.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali (NaCoNGo) wilaya ya Shinyanga Lucas Maganga akisoma risala.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali (NaCoNGo) wilaya ya Shinyanga Lucas Maganga, akiwa kwenye kikao hicho akisikiliza kwa makini.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464