Na Marco Maduhu, SHINYANGA
KIKUNDI cha kusaidiana kwenye shida na raha kiitwacho Shinyanga Chapa ya Ng’ombe, chenye makao makuu ya Ihapa Kata ya Oldshinyanga kimezinduliwa rasmi, huku Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania( SMAUJATA) wialaya ya Shinyanga ikitoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili.
Uzinduzi huo umefanyika leo Desemba 27, 2025, huku wajumbe wa kikundi wakijadili masuala mbalimbali ikiwemo rasimu ya katiba yao, kwa lengo la kuweka misingi imara ya uendeshaji na mustakabali wa kikundi hicho.
Mmoja wa walezi wa kikundi hicho, ambaye pia ni Katibu wa (SMAUJATA) Wilaya ya Shinyanga Hasna Maige, amesema anafarijika kuteuliwa kuwa mlezi, huku akitoa elimu kwao kwamba, wawe mstari wa mbele kupinga vitendo vya ukatili ndani ya jamii.
Amesema, hatarajii kuona wanakikundi hao, wakihusishwa na vitendo vya ukatili,bali wanapaswa kuwa mabalozi wazuri wa kupinga vitendo hivyo na kuwa mashujaa, kwa kuhakikisha jamii inabaki salama.
“nawaombeni sana wanakikundi cha Shinyanga chapa ya Ng’ombe muwe mashujaa wa kupinga vitendo vya ukatili, pamoja na kutoa taarifa pale mnapoona vitendo hivyo vikifanyika na siyo kunyamaza kimya, ili wahusika wachukuliwe hatua haraka,”amesema Hasna.
Aidha, amewataka wanakikundi hao kuishi kwa upendo, amani, mshikamano, na wasiingize masuala ya itikadi ya siasa, huku akiwasihi pia wahubiri masuala ya amani kwa jamii, pamoja na kushiriki kwenye maendeleo.
Mlezi mwengine Pica Chogelo, amewahasa wanakikundi hao, kuheshimu viongozi, kufuata katiba ya chama, pamoja na kutoa michango kwa wakati ili kuimarisha uhai wa chama.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikundi hicho Juma Bugohe, amesema kikundi hicho kina jumla ya wanachama 83, na kwamba pesa za michango ambazo zitakuwa zikichangwa zitakuwa salama sababu wataziweka kwenye akaunti ya kikundi, huku akiwataka wanachama washirikiane pamoja na kufuata miongozo ya katiba.
Nao baadhi ya wanachama hao, wamesema wameamua kujiunga kwenye kikundi hicho ili kusaidiana kwenye shida na raha, sababu umoja ni nguvu.
TAZAMA PICHA👇👇
Mlezi wa kikundi Shinyanga Chapa ya Ng'ombe na Katibu wa SMAUJATA Wilaya ya Shinyanga Hasna Maige akizungumza na kutoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili.
Mlezi wa kikundi Picha Chogelo akizungumza.
Mlezi wa kikundi Enock Lyeta akizungumza.
Mwenyekiti wa kikundi cha Shinyanga Chapa ya Ng'ombe Juma Bugohe akizungumza.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464