` DIWANI PUNI MHANDISI JUMANNE RAJABU ACHANGIA CHAKULA SHULE YA MSINGI BUYUBI, ATEKELEZA MAELEKEZO YA RC MHITA KUSIKILIZA VIPAUMBELE VYA WANANCHI

DIWANI PUNI MHANDISI JUMANNE RAJABU ACHANGIA CHAKULA SHULE YA MSINGI BUYUBI, ATEKELEZA MAELEKEZO YA RC MHITA KUSIKILIZA VIPAUMBELE VYA WANANCHI

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

DIWANI wa Kata ya Puni Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhandisi Jumanne Rajabu, ameahidi kuchangia magunia manne ya mahindi, mfuko mmoja wa sukari, pamoja na Sh.200,000 kwa Shule ya Msingi Buyubi ili kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula watakapo fungulia shule na siyo kusoma wakiwa na njaa.
Ametoa ahadi hiyo leo Desemba 18,2025 wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara, huku akitekeleza maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita aliyotoa jana kwenye kikao na Madiwani, kwamba wafanye mikutano ya kusikiliza vipaumbele vya wananchi.

Akizungumza kwenye mkutano huo, amesema suala la wanafunzi kusoma bila kula shuleni, hua lina muumiza sana, na katika mikakati yake kwenye Kata hiyo, ni kuhakikisha wanafunzi wote wanakula chakula shule na kusoma kwenye mazingira rafiki na kutimiza ndoto zao.
“Naomba wazazi mninunge mkono kwenye suala la kuchangia chakula shuleni, ili wanafunzi wasome wakiwa wameshiba, angalau wanywe hata uji kuliko kushinda njaa kutwa nzima, hawatazingatia masomo, mimi naanza kuchangia magunia manne ya mahidi, kiloba cha sukari na sh.200,000, awali nimeshatoa tena katika shule ya msingi Puni,”amesema Mhandisi Rajabu.

Aidha, amesema katika vipaumbele ambavyo vimetolewa na wananchi atavifanyia kazi na kuviwasilisha Halmashauri ili vipate kutekelezwa, kama maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa jana kwenye kikao chao cha Madiwani, kwamba fedha zipo za kutosha za utekelezwaji wa miradi hiyo.
Aliwashukuru pia wananchi hao kwa kumpigia kura nyingi za ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, pamoja na kura nyingi kwa Rais Samia Suluhu Hassan, na Mbunge wa Itwangi Azza Hillal Hamad.

Awali, wananchi wa kijiji cha Buyubi wakiwasilisha vipaumbele vyao kwa Diwani wao, waliomba kutekelezewa miradi ya maji, kukamilishiwa ujenzi wa Zahanati ya kijiji hicho ambayo waliinzisha kwa nguvu zao wenyewe na imefikisha miaka 18 bila ya kukamilishwa na serikali na ipo hatua ya renta, na imesha anza kuanguka.
Vipaumbele vingine ni kutekelezewa miradi ya umeme ngazi ya vitongoji, ukarabati wa miundombinu ya barabara, vivuko na ujenzi wa Stend ndogo katika njia panda ya Didia, ambapo Mabasi hupaki Barabarani na kuhatarisha usalama wa wananchi.

Mwenezi wa CCM Mkoa wa Shinyanga Richard Masele, amewaambia wananchi hao, kuwa Diwani wao anajua shida zao zote na kwamba wampatie ushirikiano na atawaletea maendeleo ya kweli.

Aidha, amewataka wananchi, kuendelea kuwaunga mkono viongozi wote walioshinda kwenye Uchaguzi Mkuu, pamoja na Rais Samia, na wasikubali kuivuruga Amani ya nchi kwa maslahi ya watu wachache wenye uchu na madaraka.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Edward Ngelela, amesema CCM wanafahamu uwezo wa diwani huyo kwenye utendaji kazi na kwamba atawahudimia wananchi vizuri kwa kutatua changamoto zao.

“Nyota njema huonekana asubuhi, diwani huyu mara baada ya kumchagua amekuja mara moja kuwashuruku, pamoja na kusikiliza vipaumbele vyenu vya miradi ya maendeleo,”amesema Ngelela.
Katika hatua nyingine amewataka wananchi, kulima mazao yanayostahimili ukame pamoja na kutunza vyakula, sababu hali ya hewa siyo nzuri na kwamba mvua zitakuwa chache.

TAZAMA PICHA👇👇
Mwenezi wa CCM Mkoa wa Shinyanga Richard Masele akizungumza.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Edward Ngelela akizungumza.
Diwani wa Kata ya Puni Mhandisi Jumanne Rajabu akizungumza kwenye mkutano huo.
Mwananchi Hamisa Mjanahel akitaja vipaumbele kwenye mkutano wa hadhara wa diwani.
Mwananchi Hamis Daudi akitaja vipaumbele kwenye mkutano wa diwani.
Mwananchi Magreth Masalu akitaja vipaumbele.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464