JINSI TANZANIA INAVYOPAA KUPITIA UCHUMI MCHANGANYIKO (MIXED ECONOMY)
Edwin Soko, Mwanza
Uchumi mchanganyiko ni mfumo wa uchumi unaochanganya vipengele vya uchumi wa soko huria (Market Economy )na uchumi unaodhibitiwa na serikali (Command Economy). Tanzania ni miongoni mwa Nchi zinazotumia mfumo huu wa uchumi, ambapo serikali na sekta binafsi hushirikiana katika uzalishaji, usambazaji wa mali na huduma, pamoja na kukuza maendeleo ya taifa. Kupitia uchumi mchanganyiko, Tanzania imepiga hatua kubwa za kiuchumi na kijamii .
Kwanza, uchumi mchanganyiko umeiwezesha Serikali ya Tanzania kusimamia na kuendeleza sekta muhimu kwa maendeleo ya taifa. Sekta kama elimu, afya, nishati, maji na miundombinu huongozwa kwa kiasi kikubwa na serikali ili kuhakikisha huduma hizi zinawafikia wananchi wote kwa usawa. Ujenzi wa barabara, reli ya kisasa (SGR), bandari na miradi ya umeme kama Julius Nyerere Hydropower Project ni mifano ya namna serikali inavyoongoza maendeleo kupitia uwekezaji wa moja kwa moja.
Pili, mfumo wa uchumi mchanganyiko umefungua milango kwa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi. Wafanyabiashara, wawekezaji wa ndani na wa nje wamepewa fursa ya kuwekeza katika sekta kama viwanda, biashara, kilimo, madini, utalii na teknolojia. Ushiriki huu umeongeza uzalishaji, ajira na mapato ya taifa. Mfano mzuri ni ukuaji wa viwanda vidogo na vya kati (SMEs) vinavyochangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa.
Tatu, uchumi mchanganyiko umechangia katika kupunguza umaskini na kuboresha maisha ya wananchi. Kupitia sera za serikali kama ruzuku za pembejeo za kilimo, mikopo kwa vijana na wanawake, pamoja na miradi ya TASAF, wananchi wengi wamepata fursa za kiuchumi na kujikwamua kimaisha. Wakati huo huo, soko huria linawahamasisha wananchi kufanya kazi kwa bidii na kuwa wabunifu ili kuongeza kipato chao.
Aidha, uchumi mchanganyiko umeimarisha uthabiti wa uchumi wa Tanzania. Wakati sekta binafsi inapokumbwa na changamoto kama mabadiliko ya soko au majanga ya kiuchumi, serikali huingilia kati kwa kuweka sera na mikakati ya kulinda uchumi wa taifa. Hali hii husaidia kudhibiti mfumuko wa bei, kulinda ajira na kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi.
Kwa ujumla, uchumi mchanganyiko umeifanya Tanzania kupaa kiuchumi kwa kuleta uwiano kati ya maslahi ya kijamii na ukuaji wa uchumi. Ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi umeongeza uwekezaji, kuboresha huduma za jamii na kuimarisha ustawi wa wananchi. Ili kuendelea kupaa zaidi, Tanzania inapaswa kuimarisha mazingira bora ya biashara, kuongeza uwajibikaji, na kuwekeza zaidi katika rasilimali watu na teknolojia kwa maendeleo endelevu ya taifa.
Serikali ya awamu ya sita (6) imejipambanua kupitia sera zake kuhakikisha uchumi mchanganyiko unawapa watanzania nafasi kubwa ya kushiriki kwenye kusukuma gurudumu la uchumi kupitia Public Private Partnership (PPP).
Uchumi huu unaileta Jamii karibu kwenye kufikiri, kuvuna na kupata faida kwenye nyanja za kibiashara chini ya usalama wa mikono salama ya Serikali, hii ni nia njema ya Serikali kwa raia wake.
Kwa maoni ya makala hii
0786349813
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464
