` ZAMA MPYA! WIZARA YA VIJANA KIPAUMBELE CHA KIZAZI KIPYA

ZAMA MPYA! WIZARA YA VIJANA KIPAUMBELE CHA KIZAZI KIPYA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Novemba 18, 2025, ameapisha Baraza jipya la Mawaziri lenye Wizara 27. 

Akitumia mamlaka yake ya kikatiba kuleta muundo mpya wa uendeshaji serikali kwa kuunda Wizara mpya ya Vijana na Mahusiano,  ni ishara ya kipaumbele kipya cha Serikali katika kushughulikia masuala ya kizazi kipya.

Wizara hiyo mpya, ambayo itakuwa chini ya Ofisi ya Rais, imekabidhiwa jukumu la kuhakikisha inashughulikia masuala ya vijana na uhusiano wao na makundi mbalimbali katika jamii ili kuleta ustawi wa kijamii. Rais Samia amemteua Mhe. Joel Nanauka (Mb) wa Mtwara Mjini kuiongoza wizara hiyo mpya.

Uundwaji wa Wizara ya Vijana na Mahusiano ni hatua muhimu ya Serikali ya Dkt. Samia kuwatuliza na kushughulikia changamoto za vijana, hasa ikizingatiwa miito mbalimbali ya hivi karibuni ya kutaka kushughulikiwa kwa masuala ya ajira, elimu, na ushirikishwaji wao katika siasa za nchi. 

Uwapo wa wizara hii unatarajiwa kutoa nguvu ya kiutendaji na rasilimali mahsusi za serikali katika kutekeleza sera zinazolenga mustakabali wa vijana.

Rais Samia pia ameonesha dhamira ya kuhakikisha shida za wananchi zinashughulikiwa haraka kwa kuunda na kupanga upya Wizara za Ofisi ya Rais kwa malengo mahususi:

Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora): Inayoongozwa na Ridhiwani Kikwete na Naibu wake Regina Ndege, inaonyesha dhamira ya kuimarisha utendaji kazi wa watumishi na maadili serikalini.

Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji): Chini ya Prof. Kitila Mkumbo na Naibu wake Pius Chaya, imeundwa kwa lengo la kurahisisha na kuharakisha mipango ya maendeleo na uwekezaji moja kwa moja kutoka ofisi kuu.

Aidha, Rais amesisitiza umuhimu wa Serikali kuwa karibu na wananchi. Hivi karibuni, Rais Samia aliwataka viongozi wote, kuanzia Mawaziri hadi Maafisa Tarafa, kuwa karibu na wananchi, kuzitambua kero zao, na kuzitatua haraka. Uteuzi huu wa Baraza unatazamwa kama njia ya kutekeleza agizo hilo kwa vitendo.

Orodha ya Baraza Jipya la Mawaziri

Rais Samia aliteua Mawaziri na Manaibu Mawaziri wapya katika Wizara zingine muhimu kama ifuatavyo:

Wizara za Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Waziri Mkuu: Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) itaongozwa na Mhandisi Hamad Masauni (Naibu: Dkt Festo Dugange). Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) itakuwa chini ya Mhe. William Lukuvi (Naibu: Ummy Nderiyananga), huku TAMISEMI ikiongozwa na Prof. Riziki Shemdoe (Naibu: Dkt Jafar Seif).

Sekta za Uchumi: Wizara ya Fedha itaongozwa na Balozi Musa Omari (Manaibu: Mhe Mshamu Munde na Mhe Laurent Luswetula). Mhe. Daniel Chongolo ni Waziri wa Kilimo (Naibu: David Silinde), na Judith Kapinga ni Waziri wa Viwanda (Naibu: Patrobas Katambi). Mhe. Dkt Ashatu Kijaji amekabidhiwa Maliasili na Utalii.

Miundombinu na Ulinzi: Dkt. Rhimo Nyansaho ndiye Waziri wa Ulinzi. Wizara ya Ujenzi inaongozwa na Mhe. Abdallah Ulega (Naibu: David Kihenzile). Mhe. Makame Mbarawa ni Waziri wa Uchukuzi.

Sekta za Jamii: Mhe. Doroth Gwajima anaongoza Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu. Mhe. Mohamed Mchengerwa ni Waziri wa Afya (Naibu: Dkt Florence Samizi), na Mhe Prof Adolf Mkenda anaongoza Elimu (Naibu: Wanu Ameir).

Wizara Nyingine Muhimu: Balozi Mahmoud Thabiti Kombo ni Waziri wa Mambo ya Nje. George Simbachawene anaongoza Mambo ya Ndani. Prof Palamagamba Kabudi ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Wachambuzi wanasema Baraza hili jipya lenye sura mpya na mseto linaashiria mabadiliko makubwa yanayolenga utekelezaji wa miradi na kufanya maamuzi yenye weledi na haki.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464