
Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Pwani, Bw. Masoud Ally, alieleza kuwa Chama chao kinalaani vikali vurugu zilizojitokeza katika maeneo machache ya mkoa wa Pwani wakati wa Uchaguzi Mkuu, akisema vitendo hivyo vilifanywa na "watu wachache wasio na nia njema na nchi hii."
Bw. Masoud alitoa tamko la wazi kuhusu wito unaoendelea wa maandamano ya Disemba 09, 2025:
"Maafisa usafirishaji wanatoa tamko kuwa hawapo tayari kushiriki kwani madhara yake ni makubwa. Kwanza, yatapelekea sisi kushindwa kufanya kazi kwa uhuru na amani, hivyo kuzorotesha uchumi wetu wenyewe, uchumi wa wateja wetu, na uchumi wa taifa kwa ujumla."
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Bw. Hemed Kibanga alikumbushia mateso waliyopitia wakati wa vurugu zilizopita.
"Kwa siku zilizotokea vurugu kila mmoja ameona tabu na mateso waliyopitia ikiwemo kukosa huduma za kijamii na baadhi ya bidhaa kupanda bei," Bw. Hemed alisema. Aliongeza kuwa hali hiyo iliathiri moja kwa moja familia zao, na kwa sababu hiyo hawapo tayari kushawishiwa tena.
Bw. Kibanga alisisitiza azma yao ya kutoa ushirikiano kamili: "Tutatoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kuwabaini wahusika na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao."
Katika hatua ya kulinda sekta yao na kuondoa wahalifu, Maafisa Usafirishaji hao wamekubaliana kuweka mfumo wa utambulisho wa wazi. Waliazimia kuvaa viakisi mwanga ambavyo vitakuwa na namba zao za usajili ili waweze kutambulika kwa urahisi. Hatua hii inalenga kuwabaini haraka wale wanaofanya uhalifu kwa kivuli cha kuwa ni maafisa usafirishaji.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464