
Mama Everina Mosses Mmari, mfanyabiashara , ametoa ushuhuda wa kuhuzunisha kuhusu hasara aliyoipata baada ya duka lake kuchomwa moto na kutoa wito mzito kwa jamii kuthamini amani na kufanya tathmini ya malezi ya vijana.
Akisimulia tukio hilo la kutisha, Mama Everina alisema vijana walivamia duka lake, kumwaga petroli, na kisha kutupa tairi la moto ndani, na hivyo kusababisha duka lote kuteketea.
"Kwa kweli sikufanikiwa kuokoa kitu chochote," alisema Mama Everina kwa masikitiko, akiongeza kuwa alikuwa wakala wa mabenki mbalimbali na kampuni za simu , simu na mashine za mabenki zimeteketea.
"Simu zote zimeungulia ndani na mtaji wangu wote umeungulia huko." Hasara hiyo ilihusu pia maduka mawili (fremu ya kwanza na ya pili) aliyokuwa ameyajaza mizigo.
Mama huyo alisisitiza kuwa vitendo hivyo haviwakilishi maandamano ya amani bali ni fujo na uhalifu.
"Yale hayakuwa maandamano ni vijana tu wametokea huko na fujo zao. Kama ni maandamano naamini maandamano huwa hayana fujo, maandamano ni ya amani."
Mama Everina alimaliza kwa kutoa wito wa dhati kwa jamii kujikita katika kulea na kushauri vijana, akisisitiza athari za matukio kama hayo kwa familia:
"Tujaribu kukaa na watoto wetu tuwashauri maisha yanaendaje kwa sababu leo ni kwangu na watoto wangu, lakini kesho ni kwa mwingine na watoto wake. Kwa kweli hili jambo linaumiza sana. Tunaomba serikali mtusaidie kuliangalia hili kwa ukaribu."
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464