
Wajasiriamali na wakazi walioathirika na vurugu wametoa onyo kali, wakisema vitendo vya kuharibu mali za watu ni uhalifu na si sehemu ya maandamano halali, na kuwataka vijana kurejea kwenye maadili ya Taifa.
Gabriel Nalika Laizer, mjasiriamali, alifafanua tofauti kati ya maandamano halali na uhalifu, akisema wale waliohusika walikuwa wanafanya uhalifu wa kawaida.
“Huu ulikuwa ni uhalifu kama uhalifu mwingine," alisema Laizer. Alieleza jinsi vurugu hiyo ilivyosababisha wizi, ikiwemo kuondoa grili za madirisha, milango, na kuiba spea za magari, hata baada ya tukio la moto kutokea.
"Maandamano ya kuja kuharibu mali za watu hasa wafanyabiashara wadogo kama sisi, si maandamano bali tunachukulia kama uhalifu mwigine," alisisitiza.
Benjamin, mkazi wa Sanawari na mfanyabiashara, aliongeza kuwa wahusika hawakuwa na nia njema, kwani walivunja maduka ya wafanyabiashara wasiohusika na maandamano.
"Hawa watu wangekuwa wana nia njema wasingefanya vurugu wengine kwa kuwavunjia maduka. Watu wengine wametumia kama fursa kuwavunjia watu maduka yao," alisema Benjamin, akitoa wito kwa mamlaka kuimarisha ulinzi.
Wito wa wadau hawa kwa vijana ni kutumia njia za kistaarabu na kisheria kutoa maoni, ikiwemo kuandika ujumbe kwenye mabango na kuepuka vitendo vyovyote vinavyohatarisha amani na mali za Watanzania wenzao.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464