` WAELEZA UMUHIMU WA WAZIRI KUANZA KWA KUKUTANA NA VIJANA KUWASIKILIZA

WAELEZA UMUHIMU WA WAZIRI KUANZA KWA KUKUTANA NA VIJANA KUWASIKILIZA


Kuundwa kwa Wizara inayojihusisha moja kwa moja na masuala ya vijana nchini ni hatua adhimu na ya kihistoria inayotoa tumaini jipya kwa kundi hili muhimu la jamii.

Hata hivyo, ili wizara hii iweze kufikia malengo yake ya msingi—hasa katika kukabiliana na changamoto kubwa ya ajira kwa vijana waliosoma—ni muhimu sana kwa Waziri anayehusika kukutana na vijana mara kwa mara. Mikutano hii si tu ishara ya upendo, bali ni mkakati wa kimuundo wa kuboresha utendaji na kutoa majibu sahihi.

Kauli hizo zimetolewa na vijana mbalimbali wakiwa katika harakati zao za kila siku jijini Dodoma.

Sospeter Chagodela alisema pamoja na kuwa faida kuu za kuwa na wizara inayoshughulika na vijana kuna haja wakati inaanza kazi Waziri kukutana na vijana ni kupata uelewa wa kina na wa moja kwa moja kuhusu hali halisi wanayokabiliana nayo.

"Serikali haiwezi kufanya maamuzi sahihi bila kujua changamoto mahususi za vijana. Kwa kukutana nao, Waziri anapata fursa ya kusikia jinsi ugumu wa kupata ajira unavyoathiri maisha yao, na hivyo, kuwezesha maisha yao.

" Waziri pia anapaswa kusikiliza mahitaji ya vijana waliosoma (walio na elimu ya juu) ambao mara nyingi changamoto yao ni tofauti na vijana wasio na elimu rasmi. Wanahitaji fursa zinazolingana na taaluma zao na uzoefu wa vitendo", alisema kijana mwingine Nazael Kirema.

Hata hivyo kuna madai kuwa mikutano ya Waziri na vijana, hasa kupitia makundi maalumu (Magroup), itafanya sera za wizara kuwa shirikishi na zenye ufanisi.

Badala ya kuunda sera kutoka ofisini, maoni ya vijana yataingizwa moja kwa moja katika: "Vijana ndio watoa maoni bora kuhusu jinsi ya kuunda miradi yenye tija na jinsi ya kuweka makundi maalumu katika maeneo ya kipaumbele kama vile kilimo biashara, TEHAMA, au viwanda vidogo

Wakiwekwa katika makundi maalumu (miradi), vijana wataweza kukopesheka kwa urahisi zaidi na wataweza kusaidiana katika kurudisha mikopo. Waziri anaweza kujua ni aina gani ya mitaji inahitajika na kwa masharti gani.

Akizungumzia umuhimu wa "Dawati la Haraka" la Msaada, Chagodela alisema vijana wengi wanapoteza matumaini kutokana na mlolongo mrefu wa urasimu. Ili wizara iweze kuwainua vijana kutoka katika hali duni (chiji) na kuwanyanyua, inahitaji mfumo wa haraka na kuwepo kwa dawati maalum, ambalo linashughulikia masuala ya vijana haraka bila mlolongo mkubwa.

"Kijana anayesaidiwa kwa haraka na kwa ufanisi anakuwa balozi wa Wizara na Serikali. Mafanikio yake huwahamasisha wengine na kuongeza imani ya vijana kwa uongozi wao" anasema kijana mwingine Nise Donald.

Kijana mwingine Zaina Muse alisema kwamba Waziri kukutana na vijana mara kwa mara ni kielelezo cha utawala bora,inasaidia kuziba pengo kati ya uongozi na wananchi, na inatoa mwelekeo wa moja kwa moja kwa Wizara ya Vijana.

"Mimi naamini jambo la msingi ni kwa wizara kuwawezesha ajira vijana waondoke na kuwa wazururaji mtaani" alisema Muse.




Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464