` WAFANYABIASHARA WADOGO WAJUA BALAA LA VURUGU, WAAHIDI KUWA MABALOZI WA AMANI

WAFANYABIASHARA WADOGO WAJUA BALAA LA VURUGU, WAAHIDI KUWA MABALOZI WA AMANI


Wakati moshi wa vurugu ukitoweka, sauti ya wananchi inaendelea kusikika ikilia kwa jambo moja: amani ni kila kitu. Miongoni mwa walioathirika zaidi na "Uchafuzi wa Amani" ni wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs), kundi linalotegemea jasho lao la kila siku kujenga familia na taifa.

Maumivu ya vurugu hizo yanaakisiwa na Bi. Evelyn Mmari, wakala wa huduma za fedha jijini Arusha, ambaye alikumbana na hasara kubwa baada ya duka lake kuteketezwa.

“Sijawahi kufikiria siku moja nitaanza upya. Nilipoteza simu, fedha, na mashine zote. Hili halikuwa maandamano, lilikuwa ni uhalifu,” alisema Bi. Mmari kwa huzuni.

Hasara hii inashuhudiwa na wengine kama Bw. Benjamin wa Sanawari. “Tulijifunza kupitia maumivu. Waliofanya vurugu hawakumdhuru kiongozi yeyote, walituharibia sisi wananchi wa kawaida,” anasema Bw. Benjamin. Kauli hii inaakisi ukweli kwamba vurugu za kisiasa huathiri moja kwa moja wananchi wa kawaida, na kusababisha mfumuko wa bei na gharama ya maisha kuwa kubwa.

Kwa mujibu wa taarifa, zaidi ya biashara 3,000 katika majiji makuu kama Dar es Salaam, Arusha, Mbeya na Mwanza ziliathiriwa. Wengine walipoteza mitaji yao yote, wengine walishindwa kulipa mikopo, na wengine wakakata tamaa. Hii inathibitisha kuwa uchumi uliyumba sana, na thamani ya amani imeonekana wazi.

Wafanyabiashara wanatambua kuwa maendeleo hayaji kwa fujo au kwa moto. Yanajengwa kwa nidhamu, uvumilivu, na ushirikiano.

Kama mfanyabiashara wa Soko la Samunge alivyosema, “Kila tunapofungua duka asubuhi, tunajua kwamba tunalinda amani yetu. Bila amani, hakuna biashara.”

Kufuatia hasara hii, wafanyabiashara wanapaswa kujitokeza na kuwa mabalozi wa amani katika jamii zao. Badala ya kulalamika mitandaoni tu, ni jukumu lao sasa,kuelimisha vijana: Kuwasisitizia wateja wao na vijana umuhimu wa utulivu. Wakiwa ndio injini ya ajira, wanapaswa kuwaongoza vijana kutumia muda wao kusaka pesa badala ya kushiriki vurugu.

Wajasiriamali na wafanyabiashara wa Tanzania leo wanajenga upya kwa moyo wa matumaini. Wameona hasara, wamepoteza mali, lakini hawajapoteza imani. Wameamua kuendelea mbele, wakijua kuwa mafanikio yanachipua kwenye udongo wa amani, si majivu ya vurugu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464