Na Marco Maduhu,SHINYANGA
NYUMBA moja imeungua na kuteketeza mali mbalimbali katika maeneo ya maduka ya Manara wa Voda Manispaa ya Shinyanga, tukio ambalo limezua taharuki na kusababisha vurugu baada ya wananchi kulishambulia gari la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, kwa madai ya kuchelewa kufika eneo la tukio.
Moto huo umezuka leo Novemba 19,2025 kwa madai ya kutokea hitilafu ya umeme, ambapo mmoja wa wapangaji, Hidaya Selemani, amesema aliwasha taa na kuona zinapiga short, na muda mfupi baadaye akaona moto ikilipuka kwenye chumba cha jirani.
Amesema alilazimika kukimbia nje na watoto wake sita huku akiomba msaada kwa kupiga kelele, ndipo wananchi wakafika na kuanza kuuzima moto huo, lakini mali zake zote zimeteketea.
“Nilikuwa nimekaa sebuleni, baadae nikaingia chumbani nilipowasha taa nikaona zinapiga short nikazima,kidogo naona moshi kwenye chumba cha jirani,ikabidi nichukue watoto wangu na kukimbia nje kuomba msaada huku moto ukiwa una wake na vitu vyangu vyote vimeteketea,”amesema Hidaya.
Mashuhuda wa tukio hilo, akwiamo Solo Bundala,wamesema kuwa licha ya wananchi kutoa taarifa kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, gari la kikosi hicho lilichelewa kufika eneo la tukio, jambo lililosababisha wananchi kuanza kuzima moto kwa kutumia ndoo za maji na kuokoa baadhi ya vitu.
“Wananchi walichukizwa na kuchelewa kufika kwa gari la Zimamoto wakati moto unateketeza mali nyingi.,ndiyo maana wengine wakalishambulia kwa mawe,” amesema Bundala.
Baby Mohamed, amesema nyumba hiyo ni ya baba yake mdogo na ina kaya tano upande wa uwani, huku sehemu ya mbele kukiwa na maduka matano ya biashara.
Kutokana na vurugu hizo, Jeshi la Polisi lililazimika kutumia mabomu ya machozi kutawanya wananchi waliokuwa wakifanya fujo na kuharibu gari la Zimamoto.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi,ambaye alifika eneo la tukio, amelaani kitendo cha wananchi kujichukulia sheria mkononi, na kuanza kulishambulia gari la Zimamoto, huku akiahidi kulinda mali za wananchi ambao wameathirika na tukio hilo Saa 24, na kubainisha hakuna mtu ambaye amedhurika na moto huo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro,naye amekemea tukio hilo la wananchi kuponda mawe gari la Zimamoto, na kuwataka vijana wawe wavumilivu kwenye matukio ya majanga, na siyo kuanza kufanya vurugu zisizo na maana na hata kusababisha kuharibu mali za umma.
Ameagiza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, kufanya tathmini ya kina kuhusu madhara na chanzo cha moto huo, akibainisha kuwa ni tukio la pili kutokea eneo hilohilo.
Aidha, ameagiza kutolewa kwa msaada wa kibinadamu kwa familia zilizoathirika na janga hilo.