Viongozi wa dini wameingilia kati kutoa wito wa maridhiano na amani, wakisisitiza kuwa mvutano wowote ule unaoendelea nchini unapaswa kukomeshwa kwa njia ya mazungumzo na umoja."Tukunjue mioyo, na hatustahili kuvutana, tukae chini," alisema Askofu Mpembwa, akisisitiza kuwa nchi hii ni mali ya Watanzania wote.
Askofu Mpembwa alionyesha faraja kutokana na ishara za maridhiano zilizotolewa na viongozi wa juu, akimrejelea Rais: "Faraja niliyoipata, Mama amekunjua moyo, ametaka tukae tufikie makubaliano. Nchi hii ni ya kwetu wote."
Hata hivyo, alionya vikali kuhusu hatari ya kuendelea kwa mvutano: "Hili la tuendelee kuvutana au tukae chini si sawa kwani mara zote kukitokea tatizo na watu katika makundi wakaanza hatukubali, tutaona, tukifikia hapo, tutaharibu nchi."
Aliongeza kuwa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonyesha kuumizwa na yaliyotokea na kuweka wazi hisia zake, hivyo ni muhimu pande zote zikakubali kukaa mezani bila mashinikizo ya aina yoyote.
Rais Samia alitoa pole zake kwa familia zote zilizopoteza ndugu na jamaa zao kwenye maandamano ya Oktoba 29, akionyesha masikitiko yake wakati wa hotuba ya kufungua Bunge la 13.
Kiongozi huyo wa dini alikiri kwamba matukio hayo ya vurugu yameumiza, yamesikitisha, na kuchafua sana Tanzania. "Wengine wameumia, wengine wapo ndani na wameachiwa, lakini je, tuendelee kukaa hapa?" alihoji.
Aliwataka hasa vijana kutafakari hatari ya kutokuwa na nia ya maridhiano: "Labda chama cha siasa au wenyewe Gen Z, tukiwa na fikira kama hizo, tutalipeleka taifa mahali pasipofaa."
Wito wa Askofu Mpembwa ulipokewa kwa maoni mbalimbali, huku baadhi ya Watanzania wakisisitiza umuhimu wa kushughulikia mizizi ya matatizo.
Pamoja na wito huo, wananchi wengi walipongeza viongozi wa dini kwa kusimama kama kiungo imara cha umoja, huku wakikumbusha kuwa amani ni zawadi ya thamani ambayo inategemea majadiliano hata pale kunapotokea kukwazana.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464