` MSISITIZO WA KISHERIA BAADA YA OKTOBA 29: SERIKALI YAONYA UCHOCHEZI DESEMBA 9

MSISITIZO WA KISHERIA BAADA YA OKTOBA 29: SERIKALI YAONYA UCHOCHEZI DESEMBA 9


Kufuatia madhara makubwa yaliyosababishwa na vurugu za Oktoba 29, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa onyo kali na msisitizo kuhusu wajibu wa kisheria wa kila raia na hatua zitakazochukuliwa dhidi ya wachochezi.

Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari aliweka wazi kuwa Serikali haiwezi kuvumilia vitendo vya uvunjifu wa amani chini ya kivuli chochote, hasa ikizingatiwa vitisho vinavyoendelea kuhusu Desemba 9.

"Vyombo vya ulinzi na usalama vimeagizwa kuwa macho masaa 24 na vitachukua hatua kali na za haraka kwa mujibu wa sheria dhidi ya mtu au kundi lolote linalojaribu kuhujumu amani ya nchi. Uchochezi kupitia mitandao ya kijamii unachukuliwa kuwa kosa la jinai," alisema.

Kauli hii inalenga kuwasisitiza Watanzania, hasa vijana, kujiepusha na maneno ya kiuchochezi yanayoweza kusababisha amani kutoweka, kwani sheria haitamwacha salama yeyote atakayejaribu kuhatarisha uhai wa nchi.

Abdallah Vincent Machali, kijana aliyeshuhudia athari za vurugu, alikumbusha jinsi gani amani inavyohusiana moja kwa moja na huduma za msingi, akionyesha kuwa uhalifu wa vurugu una gharama kubwa sana kwa jamii.

"Huduma za chakula zilikosekana. Mkate ule uliadimika kwelikweli... Tumeathirika kwa kiasi kikubwa sana... Sidhani tena kuwa kuna kijana mwenye akili timamu nchini atajitokeza tena kufanya vurugu Desemba 9."

Ushuhuda wake unasisitiza hoja kuwa hakuna maisha bila amani. Kukosekana kwa amani huathiri moja kwa moja upatikanaji wa bidhaa muhimu kama nyanya, mkate, na hata kuharibu sekta ya elimu.

Naye Askofu Dkt. Cyprian Hilinti alisisitiza kuwa amani ndiyo inawezesha shughuli za kijamii na kiuchumi. Aliongeza kuwa kazi na ibada haziwezi kufanyika iwapo kutakuwa na mabomu na risasi.

Wakati waumini na wananchi wakisisitiza kuwa amani ni fahari na urithi unaopaswa kulindwa, pia wanatoa wito wa: "Tudumishe amani yenye haki ndani yake kwa kila Mtanzania."

Hii inamaanisha kuwa jukumu la kulinda amani linaenda sambamba na jukumu la Serikali kushughulikia mizizi ya matatizo ili kuleta uponyaji wa jamii, na wakati huo huo Sheria zichukuliwe dhidi ya wachochezi na vijana wanaotaka kuleta vurugu.

Kijana moja alisema kila Mtanzania anapaswa kusaidia Serikali katika kukemea na kuripoti dalili zote za uchochezi ili kuhakikisha Desemba 9 na siku zinazofuata zinapita kwa utulivu na kuwezesha Taifa kuendelea na safari yake ya maendeleo.



 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464