` RC MHITA APONGEZA UONGOZI MPYA WA KANISA LA WASABATO NGBF MKOANI SHINYAGA

RC MHITA APONGEZA UONGOZI MPYA WA KANISA LA WASABATO NGBF MKOANI SHINYAGA


Na Johnson James,SHINYANGA

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, leo amekutana na kupongeza uongozi mpya wa Kanisa la Wasabato la Nyanza Gold Belt Field (NGBF) waliofika ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha rasmi baada ya kuchaguliwa kuongoza kanisa hilo kwa kipindi cha miaka mitano.
Katika salamu zake, Mhe. Mhita aliwapongeza viongozi hao kwa dhamana waliyopewa na waumini wao, akiwataka kuwaongoza kwa hekima, maadili na uadilifu mkubwa. Alisisitiza kuwa uongozi wao unapaswa kuacha alama ya mshikamano, upendo na amani miongoni mwa waumini wao na jamii kwa ujumla.

“Ni matarajio yangu kwamba mtaendelea kuwa sehemu ya kuhakikisha jamii inakuwa imara kiroho na kijamii. Mkawe kielelezo chema kwa waumini wenu na jamii,” alisema RC Mhita.
Aidha, alibainisha kuwa Mkoa wa Shinyanga uko salama na shughuli za wananchi zinaendelea kama kawaida, huku akisisitiza kuwa maeneo yaliyowahi kuwa na changamoto za kiusalama kama Wilaya ya Kahama sasa yameimarishiwa ulinzi kwa ushirikiano na vyombo vya dola ili kuhakikisha ustawi wa kiuchumi unaendelea.

Viongozi waliochaguliwa kuongoza NGBF kwa miaka mitano ni Mch. Shukrani Mutaki Askofu Mkuu, NGBF, Mch. Joshua Mbwambo Katibu Mkuu, NGBF, ELD. Padon Kikiwa Mhazini Mkuu, NGBF.
Kwa upande wake, Mch. Joshua Mbwambo ambaye ni Katibu Mkuu wa NGBF, alitoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa kwa ukaribisho na ushirikiano aliouonesha kwa viongozi wa dini.

“Tunamshukuru sana Mkuu wa Mkoa kwa kutupokea na kutupa maneno ya kututia moyo. Tunaahidi kuendeleza ushirikiano na Serikali na kuwa sehemu ya kuhimiza maadili mema, amani na maendeleo miongoni mwa waumini na jamii ya Shinyanga,” alisema Mch. Mbwambo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464