` VYAMA VYA UPINZANI SHINYANGA VYATOA TAMKO KUSHIRIKIANA NA SERIKALI YA AWAMU YA SITA

VYAMA VYA UPINZANI SHINYANGA VYATOA TAMKO KUSHIRIKIANA NA SERIKALI YA AWAMU YA SITA


Na Marco Maduhu, SHINYANGA

VYAMA saba vya upinzani mkoani Shinyanga, vimetangaza kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na kuahidi kutoa ushirikiano katika kusukuma maendeleo ya wananchi.

Vyama hivyo vimetoa msimamo huo leo Novemba 18, 2025 wakati wa mkutano na waandishi wa habari, huku vikilaani vurugu zilizojitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 na kuwataka Watanzania kulinda amani ya nchi.
Mratibu wa Chama Makini Kanda ya Ziwa, Mohamed Msanya, amesema Uchaguzi Mkuu uliopita umesimamiwa kwa misingi ya demokrasia na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ambapo kila chama kilipata haki sawa ya kushiriki, na kutamka kuunga mkono Serikali ya awamu ya Sita.

Amesema wanatambua mchango wa viongozi wote waliochaguliwa kuanzia ngazi ya Udiwani, Ubunge na Urais, na kusisitiza kuwa watashirikiana nao katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CHAUMMA Mkoa wa Shinyanga, Rashid Katabanya, amelaani vurugu na matukio ya uvunjifu wa amani yaliyoshuhudiwa katika uchaguzi huo na kuwataka wananchi kutokubali kutumiwa kwa manufaa ya wachache.

“Tunapaswa kuilinda tunu yetu ya amani. Hakuna maendeleo yatakayopatikana iwapo nchi itakuwa kwenye vurugu zisizo na msingi,” amesema Katabanya.
Naye Rehema Bulila kutoka Sauti ya Umma (SAU), amesema hotuba ya Rais Samia aliyoitoa bungeni imeleta matumaini mapya kwa Taifa, hususan kwa vijana, kutokana na kuanzishwa kwa Wizara ya Vijana itakayoshughulikia kwa karibu changamoto zao.

Amesisitiza vijana wasikubali kutumiwa kuvuruga amani wakati serikali tayari imeweka mazingira ya kutatua changamoto zinazowakabili.
Vyama vilivyotoa tamka la pamoja ni CHAUMMA, NLD, AAFP, SAU, UND,DP na CCK.

TAZAMA PICHA👇👇
Mratibu wa Chama Makini Kanda ya Ziwa, Mohamed Msanya akizungumza.
Mwenyekiti wa CHAUMMA Mkoa wa Shinyanga, Rashid Katabanya akizungumza.
Rehema Bulila kutoka Sauti ya Umma (SAU),akizungumza.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464