` WANANCHI SHINYANGA KUONGEZEKA HADI MILIONI 4.4 IFIKAPO 2050,KUTOKA MILIONI 2.2

WANANCHI SHINYANGA KUONGEZEKA HADI MILIONI 4.4 IFIKAPO 2050,KUTOKA MILIONI 2.2

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

Idadi ya wakazi wa Mkoa wa Shinyanga inatarajiwa kuongezeka maradufu na kufikia zaidi ya watu milioni 4.4 ifikapo mwaka 2050, kutoka milioni 2.2 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 18, 2025 na Meneja wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Mkoa wa Shinyanga, Eriud Kamendu, wakati akiwasilisha taarifa ya makadirio ya idadi ya watu katika maadhimisho ya siku ya Takwimu Afrika Kanda ya Magharibi yaliyofanyika mkoani humo.
Amesema,idadi ya watu katika Mkoa wa Shinyanga inaongeze kwa kasi,ambapo kwa makadirio ifikapo mwaka 2050 kutakuwa na watu wapatao milioni 4.4, kutoka milioni 2.2, na kwamba wanaume watakuwa milioni 2.201 na Wanawake milioni 2.24.

“Makadirio haya yanaonyesha kuwa idadi ya watu katika Mkoa wa Shinyanga inakua kwa kasi ikionekana kuongezeka kutoka watu milioni 2.3 mwaka 2023 hadi kufika watu milioni 4.4 mwaka 2050 ambapo idadi ya watu katika Mkoa huo itaongezeka maradufu kwa kipindi cha miaka 22 ijayo,”amesema Kamendu.
Aidha, Kaimu Meneja Takwimu Mkoa wa Kigoma, Hemed Nkunya, akiwasilisha taarifa ya pato la Mkoa wa Shinyanga, amesema Shinyanga inashika nafasi ya 17 kwa uchangiaji wa Pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 3, huku pato la mtu mmoja likikadiriwa kufikia Sh. milioni 2.3 kwa mwaka.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, alisema takwimu sahihi ni msingi wa maendeleo na mpangilio mzuri wa huduma za kijamii, hususan serikali inapopanga bajeti na uwekezaji kulingana na ongezeko la idadi ya watu.
Amesema makadirio hayo ya ongezeko la idadi ya watu katika mkoa wa Shinyanga kufika watu milioni 4.4 ifikapo mwaka 2050 kutoka milioni 2.2 mwaka 2022, kwamba takwimu hizo itaisaidia serikali kupanga mipango yake ya maendeleo kwa muda mrefu.

Aidha,ameitaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuendelea kuzalisha takwimu sahihi kwa ajili ya mipango ya maendeleo ya taifa, na kwamba bila takwimu sahihi,maendeleo hayawezi fika kwa wananchi kwa kuzingatia usawa kulingana na idadi ya watu.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, CP Salum Hamdun, amesema maadhimisho hayo yameshirikisha mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Kigoma na Tabora kwa lengo la kuongeza uelewa juu ya mchango wa takwimu katika maendeleo ya nchi.

Maadhimisho hayo yamebeba kaulimbiu isemayo: “Kuongeza ubunifu katika matumizi ya takwimu na taarifa ili kujenga jamii jumuishi inayojali haki, amani na maendeleo kwa Waafrika.”

TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamdun akizungumza.
Morice Mlilo kutoka NBS Makao Makuu akizungumza.
Meneja Takwimu msaidizi Mkoa wa Shinyanga Unambwe Erasto akiwasilisha majukumu ya NBS.
Kaimu Meneja Takwimu Mkoa wa Kigoma Hemed Nkunya akiwasilisha Pato la Mkoa wa Shinyanga.
Meneja Takwimu Mkoa wa Shinyanga Eriud Kamendu akiwasilisha makadirio ya Idadi ya watu Mkoa wa Shinyanga kwa mwaka 2023 hadi 2050.
Maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika 2025 yakiendelea katika Mkoa wa Shinyanga.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464