
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameunda Tume Huru ya Uchunguzi kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, huku akimteua Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande Othmani, kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo.
Uteuzi huo umefanywa kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo Rais chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32.
Wajumbe Maarufu Walioteuliwa
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka, imetaja orodha ya wajumbe wa Tume hiyo, wakiwemo wataalamu na viongozi wastaafu wenye uzoefu mkubwa kitaifa na kimataifa:
Profesa Ibrahim Juma: Jaji Mkuu mstaafu wa Mahakama ya Tanzania.
Balozi Ombeni Sefue: Mwanadiplomasia na Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu.
Balozi Radhia Msuya: Mwanadiplomasia na Balozi mstaafu.
Paul Meela: Mwanadiplomasia na Balozi mstaafu.
Said Mwema: Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) mstaafu.
Balozi David Kapya: Mwanadiplomasia na Balozi mstaafu.
Dk. Stergomena Tax: Aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Ahadi ya Maridhiano na Amani
Uundwaji wa Tume hii unatekeleza ahadi ya Rais Samia aliyoitoa hivi karibuni wakati akifungua Bunge la 13. Lengo kuu ni kujua kiini cha tatizo, kubaini wahusika waliochochea vurugu hizo, na kutumia matokeo ya uchunguzi huo kama mwanzo wa mchakato wa mazungumzo na maridhiano ya kitaifa.
"Serikali imechukua hatua ya kuunda tume kuchunguza yaliyotokea ili tujue kiini cha tatizo na taarifa itakayotolewa na tume hiyo, itatuongoza katika mazungumzo ya kuleta amani na maelewano nchini,” alisema Rais Samia.
Rais pia alitoa pole kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao na waliojeruhiwa, akionyesha kuhuzunishwa na matukio hayo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464