` MISA-TANZANIA: HATUTAKUBALI KUCHONGANISHWA NA MTU YEYOTE KATI YA WAANDISHI WA HABARI NA WANANCHI

MISA-TANZANIA: HATUTAKUBALI KUCHONGANISHWA NA MTU YEYOTE KATI YA WAANDISHI WA HABARI NA WANANCHI

Na Marco Maduhu,DODOMA

TAASISI ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN), imewataka waandishi wa habari nchini kuendelea kusimamia maadili ya taaluma yao na kutokubali kuchonganishwa na mtu yeyote katika uhusiano wao na wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa leo Novemba 27,2025 na Mwenyekiti wa MISA-TAN Edwin Soko, wakati akitoa neno kwenye ufunguzi wa mafunzo ya uandishi wa habari za amani yaliyoshirikisha waandishi 100 kutoka mikoa mbalimbali.

Soko amesema waandishi wa habari ni daraja muhimu linalounganisha Serikali na wananchi,hivyo wanapaswa kuendelea kuwa mstari wa mbele kudumisha amani, utulivu na mshikamano nchini.
“Vyombo vya habari ni nguzo kubwa ya usalama wa Taifa, Sisi kama waandishi hatutakubali kuyumbishwa, kutikiswa au kuelekezwa na mtu yeyote mwenye lengo la kutuchonganisha na wananchi. Tutaendelea kusimamia maadili, weledi na uzalendo,” amesema Soko.

Ataja tukio la Oktoba 29

Aidha,amesema kilichotokea Oktoba 29 watu wote wamesikitishwa, na hata tasnia ya habari iliguswa kwa wapendewa wao kupoteza maisha,kujeruhiwa na kupoteza vifaa vya kazi,huku akiomba Wizara ya Mambo ya ndani iendelee kulinda amani ya nchi pamoja na kuwahakikishia waandishi wa habari ulinzi na usalama wakati wa majukumu yao.

“Waandishi wa habari Tanzania ni Wazalendo na siyo wasaliti na tutaendelea kufanya kazi zetu kwa kuzingatia weledi na maadili, na tuna muunga mkono Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kauli yake kwamba ni wakati sasa wa kujenga umoja,mshikamano na upendo na sisi tutaendelea kuandika habari za kuhimiza amani ya nchi,”amesema Soko.

Mafunzo yaongeza weledi.

Aidha,ametaja faida za mafunzo hayo, kwamba waandishi wa habari wanajengewa weledi na uwezo mkubwa wa kuandika habari za kuhamasisha amani, kupunguza taarifa za uchochezi, upotoshaji, kuchambua habari za kuchochea migogoro, na kuandika habari za kuhamasisha umoja amani na mshikamano wa taifa.
Serikali yaahidi ulinzi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Dennis Lazaro Londo, ameipongeza MISA Tanzania kwa kutoa mafunzo hayo ya Uandishi wa Habari za Amani, kwamba ni ya muhimu sana, katika kuimarisha amani ya nchi.

Amesema mafunzo hayo yametolewa katika muda muafaka ambapo taifa linawahitaji sana waandishi wa habari, kutokana na kupita kwenye kipindi kigumu kwa yaliyotokea Oktoba 29, kwa kuwapatia habari sahihi zenye kulinda na kuimarisha amani ya nchi.

“Misa Tanzania ni mdau mwaninifu kwa serikali hata katika nyakati ambazo imezipitia, na huo ndiyo uzalendo ambao tunautaka kwa maslahi ya taifa letu,”amesema Londo.

Amesema Waandishi wa habari wanajukumu la kulinda amani, utulivu na umoja, huku akivipongeza vyombo vya habari kwa kutoa habari nyingi za kusisitiza amani kupitia viongozi wa dini, na Jeshi la Polisi.

“Amani ni muhimu sana,nje na amani ni vigumu kufanya jambo lolote lile, hivyo Tasnia hii ya habari ni muhimu sana katika kudumisha amani ya nchi,”ameongeza.
Aidha, ameahidi kuwa Wizara hiyo itaendelea kulinda usalama wa Waandishi wa habari na vifaa vyao vyote, wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

UTPC yaipongeza MISA-TAN

Mwenyekiti wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Kenneth Simbaya, aliishukuru MISA-TAN kwa kuandaa mafunzo hayo, akisema ni chachu ya kuimarisha umoja na kuunganisha Taifa.

TAZAMA PICHA👇👇
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Dennis Lazaro Londo akizungumza.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Dennis Lazaro Londo akizungumza.
Mwenyekiti wa MISA-TANZANIA Edwin Soko akizungumza.
Mwenyekiti wa MISA-TANZANIA Edwin Soko akizungumza.
Mwenyekiti wa UTPC Kenneth Simbaya akizungumza.
Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa TCRA Robin Ulikaye akizungumza.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania DCP David Misime akizungumza.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464