` MAHAFALI YA 45 VETA SHINYANGA YAFANA

MAHAFALI YA 45 VETA SHINYANGA YAFANA


MAHAFALI YA 45 VETA SHINYANGA YAFANA

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MAHAFALI ya 45 ya Daraja la Pili katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mkoani Shinyanga yamefana, huku wahitimu wakihimizwa kuitumia elimu ya ujuzi waliyoipata katika kujiendeleza na kuendesha maisha yao.
Sherehe hizo zimefanyika leo Novemba 21, 2025, chuoni hapo, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Jambo na Mbunge wa Jimbo la Meatu Salum Khamis, aliyewakilishwa na Salehe Mohamed.

Akizungumza kwa niaba ya Mbunge Khamis, Mohamed amewataka wahitimu kutumia ujuzi walioupata VETA katika kujiajiri na kuchangamkia fursa za uzalishaji mali.
“Nawapongeza sana kwa kumaliza mafunzo na kupata ujuzi. Elimu hii kaitumieni vizuri ili muweze kuendesha maisha yenu,” amesema Salehe.

Amesema changamoto zilizowasilishwa na uongozi wa chuo atazifikisha kwa mhusika ili zitafutiwe ufumbuzi.

Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga, Abraham Mbughuni, amesema chuo kimeendelea kufanya vizuri kwa kutoa wahitimu wenye ujuzi wa hali ya juu, ambao wengi wao wameajiriwa katika migodi mikubwa na viwanda mbalimbali.

Amebainisha kuwa kwa upande wa fani ya mitambo mizito, nchi za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi zimekuwa zikitegemea sana chuo hicho.
Aidha, Mbughuni ameomba kuungwa mkono katika ujenzi wa uzio chuoni hapo kwa ajili ya usalama wa wanafunzi na mali za chuo, na kwamba sasa hivi inajengwa Stand ya Mabasi ya Mkoa jirani na Chuo hicho,na hivyo kuhofia usalama wao.

Pia, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha elimu na kujenga vyuo vya VETA katika kila wilaya nchini.
Msajili wa Chuo hicho Rashid Ntahigiye, amesema chuo kina jumla ya fani 10 za muda mrefu na fani 35 za muda mfupi, na sasa wanajumla ya wanafunzi 518.

Katika risala ya wahitimu iliyosomwa na Stephen Kasongo, amesema wamehitimu jumla ya wanafunzi 152, wasichana 54 na wavulana 98.

TAZAMA PICHA👇👇
Salehe Mohamed akimwalisha Mkurugenzi wa Jambo na Mbunge wa Meatu Salum Khamis kwenye Mafahali VETA.
Salehe Mohamed akimwalisha Mkurugenzi wa Jambo na Mbunge wa Meatu Salum Khamis kwenye Mafahali VETA.
Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga, Abraham Mbughuni akizungumza.
Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga, Abraham Mbughuni akizungumza.
Msajili wa Chuo cha VETA Shinyanga Rashid Ntahigiye akisoma taarifa ya Chuo.
Stephen Kasongo akisoma Risala ya Chuo.
Mahafali yakiendelea.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464