`
Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa , Oktoba 18, 2025, na kusainiwa na Paul Mselle, msemaji wa Idara hiyo, tukio hilo lilitokea katika Kituo cha Uhamiaji cha Sirari, mkoani Mara, ambapo Heche alivuka mpaka na kuingia nchini Kenya kinyume na masharti ya Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54.
“Idara ya Uhamiaji inapenda kuujulisha umma kuwa leo tarehe 18 Oktoba, 2025, katika Kituo cha Uhamiaji cha Mpaka wa Sirari mkoani Mara, Mheshimiwa John Wegesa Heche ameondoka nchini kwa kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani bila kufuata taratibu na kanuni za uhamiaji zilizoundwa chini ya Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, Idara hiyo imetoa wito kwa Watanzania na wageni wanaotoka au kuingia nchini kuhakikisha wanafuata taratibu zote za kisheria zinazohusu uingiaji, ukaaji na utokaji wa watu nchini, ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria.
Taarifa hii imekuja saa chache baada ya Chadema kudai kuwa Heche amezuiwa kusafiri kwenda nchini Kenya kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, yanayotarajiwa kufanyika Oktoba 19, 2025, kijijini Bondo.