` CHIFU LUKWELE WA WALUGURU AHIMIZA KIZAZI KIPYA KUJIEPUSHA NA SIASA ZA VURUGU

CHIFU LUKWELE WA WALUGURU AHIMIZA KIZAZI KIPYA KUJIEPUSHA NA SIASA ZA VURUGU

 

Na Mwandishi Wetu

Wakati mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2025 ukiendelea, Mmoja wa viongozi wa kimila nchini, Chifu Mussa Bwakila Lukwele IV, ametoa wito mzito kwa Watanzania, hasa kizazi kipya, kulinda na kuienzi amani iliyoisukuma Tanzania kuwa 'Kisiwa cha Amani' barani Afrika.

Chifu Lukwele, ambaye ni Chifu Mkuu (Paramount Chief) wa Waluguru wa Himaya ya Jadi ya Choma, amempongeza kwa dhati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia misingi imara ya upendo, umoja, utulivu, na mshikamano iliyoachwa na watangulizi wake.

Akirejelea tafiti za hivi karibuni za taasisi za kimataifa, ikiwemo Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Chifu Lukwele alibainisha kuwa Tanzania imeng'ara kwa kuwa nchi salama zaidi Afrika Mashariki.

"Bila hiyana hatuna budi kumpongeza Mkuu wa nchi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kusimamia misingi iliyopo awamu zote," alisema Lukwele.

Ripoti hizo zimeiweka Tanzania katika nafasi nzuri, huku ikielezwa kuwa ina viwango vichache vya uhalifu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, hali inayotufanya kuwa 'Barua Inayosomeka' kwa mataifa mengine. Utafiti wa Global Peace Index (GPI) wa 2025 pia unaiorodhesha Tanzania katika nafasi ya 73 kwa kuwa nchi salama zaidi duniani.

Onyo kwa ‘Kizazi Z’ Dhidi ya Siasa za Uhasama

Akihofia hali ya sasa ya kisiasa, Chifu Lukwele alielekeza wito maalum kwa vijana wa kizazi kipya (‘Generation Z’), ambao hawajawahi kushuhudia vita, akiwasihi 'wasichukulie poa' neno vita.

"Vijana wachache kizazi hiki hawajui nini maana ya machafuko, tunawasihi wasikubali kushawishiwa na wanasiasa wasiolitakia mema Taifa hili," alisema, na kuwasihi vijana watazame hali ilivyo kwa majirani zetu, ambapo Tanzania imebaki kuwa 'kimbilio la walioharibikiwa'.

Alisisitiza kuwa kizazi kichanga kipo hatarini kuburuzwa kwenye giza kutokana na uzoefu mdogo wa maisha na upeo finyu wa kuchanganua mambo.

Maisha Baada ya Uchaguzi na Siasa za Hoja

Chifu Lukwele alikemea wanasiasa wanaotumia matatizo ya vijana, ikiwemo ukosefu wa ajira au mitaji, kuwachochea wavuruge amani kwa maslahi yao binafsi ya kisiasa.

Aliwataka wanasiasa kutumia kipindi hiki cha kampeni kunadi sera na kujenga hoja zenye kuingia akilini mwa wapiga kura, badala ya kupanda mbegu za chuki, uhasama, mifarakano, na kushambuliana binafsi.

"Ikumbukwe kuwa, KUNA MAISHA BAADA YA UCHAGUZI ambayo ni marefu zaidi kuliko miezi miwili ya kampeni na siku yenyewe ya kupiga kura," alisisitiza Chifu Lukwele.

Majirani Watikisika: Kenya na Uganda Zatajwa Kushuka

Kinyume na hali ya Tanzania, ripoti za kimataifa zinaonesha majirani wamekuwa na hali mbaya ya usalama:

Kenya: Inaongoza kwa kutokuwa salama Afrika Mashariki, ikiorodheshwa nafasi ya 14 barani Afrika.

Uganda: Imetajwa nafasi ya 23 kwa nchi isiyo salama, na kuifanya ya pili katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Aidha, ripoti ya GPI inaeleza kuwa kiwango cha amani Kusini mwa Jangwa la Sahara kimepungua kwa wastani, huku nchi tatu kati ya kumi zenye migogoro mikubwa zaidi duniani zikipatikana kwenye eneo hili. DRC, Sudan Kusini, Mali, Burkina Faso, Somalia, CAR, na Nigeria zimetajwa kuwa miongoni mwa mataifa saba (7) yenye hali mbaya zaidi ya usalama barani Afrika.

Wito wa Kuelimisha Kuanzia Familia

Ili kudumisha hali hii ya kipekee ya amani, Chifu Lukwele alihitimisha kwa kutoa wito kwa kila Mzazi na Mlezi: "Sema na Mwanao."

Alisisitiza kuwa jitihada za Rais Samia za kulinda amani hazina budi kuungwa mkono kwa kutoa elimu kubwa zaidi kwa kundi la vijana, kuanzia ngazi ya familia, ili kuwawezesha kutambua matokeo mabaya ya vurugu na kukataa kuburuzwa na siasa za uchochezi.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464