` UCHAGUZI 2025: KUPIGA KURA NDIO 'SILAHA YA DEMOKRASIA'

UCHAGUZI 2025: KUPIGA KURA NDIO 'SILAHA YA DEMOKRASIA'

 




Pamoja na Tanzania kuweka rekodi mpya ya kihistoria baada ya wapiga kura zaidi ya milioni 37.6 kujiandikisha kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 – idadi kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi,idadi hii kubwa inatajwa na wachambuzi kama ishara ya imani kubwa ya Watanzania katika mfumo wa kidemokrasia na amani.

Huku tarehe ya kupiga kura ikikaribia, Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) imethibitisha kuwa hamasa ya wananchi kushiriki katika kutimiza wajibu wao wa Kikatiba ni kubwa.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 5(1), inampa kila raia mwenye umri wa miaka 18 na zaidi haki ya msingi ya kupiga kura. Aidha Kauli za wananchi waliohojiwa zimeonyesha utambuzi wa kina wa umuhimu wa haki hii.

Mkazi wa Goba mkoani Dar es salaam,John James amesisitiza umuhimu wa kila mtu kushiriki: “Kupiga kura ni haki ya msingi. Ukikosa kupiga kura, unampa mwingine ruhusa ya kukuamulia kiongozi. Ni wajibu wetu kila mmoja kwenda kupiga kura kwa maendeleo ya nchi yetu.”

Khadija Suleiman, Mama Lishe kutoka Gongolamboto, anaelezea matarajio yake ya mabadiliko kupitia sanduku la kura: "Nitapiga kura Oktoba 29 kuchagua viongozi wanaojua shida za wananchi kama sisi. Tunataka viongozi wanaojali barabara, maji na mikopo kwa wanawake."

Kauli hizi zinadhibitisha kuwa Watanzania wanaona kura kama njia halali na ya amani ya kudai mabadiliko na maendeleo, na si kupitia maandamano, vurugu, wala jazba.

Tanzania: Nguzo ya Amani Afrika

Tanzania imejijengea heshima kubwa kimataifa kama mfano wa demokrasia barani Afrika, hasa kwa uwezo wake wa kuendesha chaguzi kwa amani, utulivu na utawala wa sheria.

Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa dhamira hii ya Watanzania kutimiza wajibu wao kwa amani inathibitisha kuwa: "Watanzania hawatapigana; watapiga kura."

Kwa kuwa kura ni silaha muhimu ya kidemokrasia, Serikali na wadau wa demokrasia wamewataka Watanzania wote—vijana, wazee, wafanyabiashara, na wakulima—kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, kupiga kura kwa utulivu, na kisha kurudi majumbani kwa heshima ya taifa.

Kura yako ni sauti yako. Sauti yako ni nguvu ya taifa. Usiiache.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464