` MIPANGO YA SERIKALI KULETA NAFUU BEI YA GESI

MIPANGO YA SERIKALI KULETA NAFUU BEI YA GESI

 

Serikali ya Tanzania imeongeza kasi ya juhudi zake za kupeleka gesi asilia kwa njia ya bomba moja kwa moja majumbani, ikisisitiza kuwa mradi huo ndio suluhisho la kudumu la kufanya nishati hiyo kuwa nafuu zaidi kwa Watanzania. 

Wizara ya Nishati na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) zimeeleza wazi kuwa lengo kuu si kupunguza bei za mitungi ya gesi, bali ni kuondoa kabisa hitaji la mitungi hiyo kwa kuwekeza katika miundombinu ya bomba.

Kauli hiyo inatolewa huku Miradi ya kuunganisha gesi moja kwa moja majumbani inaendelea. Katika Jiji la Dar es Salaam, kwa mfano, TPDC inatekeleza mpango wa kuunganisha nyumba zaidi ya 1,000 na mtandao huo.

Juhudi hizi za Serikali za kusambaza gesi zinakwenda sambamba na ahadi zilizotolewa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya 2020-2025, ambayo inaitaja gesi asilia kama "injini ya maendeleo ya Tanzania" na chanzo cha nishati safi.

Aidha Katika baadhi ya maeneo kama Lindi, wateja wa awali wamepata fursa ya kuunganishiwa gesi bure ili kuondoa mzigo wa gharama kubwa za kuanzisha matumizi ya nishati hiyo.

Kwa mujibu wa Serikali, gesi asilia inayotumika kwa njia ya bomba huishia kuwa nafuu zaidi kuliko nishati nyingine, huku ikipunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa.

Hata hivyo, kuelekea uchaguzi mkuu, kumekuwa na malalamiko mengi katika mitandao ya kijamii na mitaani yanayotaka Serikali itilie mkazo zaidi kwenye bei ya sasa ya gesi ya mitungi (LPG).

Wananchi wengi wamekuwa wakiomba bei za gesi, hasa mitungi midogo ya kujaza, ishuke hadi kufikia kiwango cha chini, wakisisitiza kuwa nchi yenye rasilimali nyingi za gesi haipaswi kuuza nishati hiyo kwa bei ghali kiasi hicho.


Serikali imesisitiza kuwa matumizi ya ndani yamepewa kipaumbele, na kiasi kikubwa cha gesi asilia (trilioni 1.3 kati ya futi za ujazo trilioni 57.54) kimetengwa kwa matumizi ya miaka mingi ijayo, na hivyo kuahidi mustakabali mwema wa nishati hiyo kwa Watanzania.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464