` MAMBO BAM BAM TANGA – MAADHIMISHO YA SIKU YA CHAKULA DUNIANI KITAIFA

MAMBO BAM BAM TANGA – MAADHIMISHO YA SIKU YA CHAKULA DUNIANI KITAIFA

 

Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kitaifa mwaka huu yanafanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Usagara, jijini Tanga yakihusisha mashindano ya ubunifu katika mapishi ya mazao ya asili yaliyosahaulika au kutotiliwa mkazo katika milo ya familia.

Mashindano hayo yanatarajiwa kudumu kwa muda wa siku tatu, ambapo washiriki wataonyesha ubunifu wao katika kupika mazao ya choroko, mbaazi na dengu. Kila zao litapikwa kwa aina tatu za milo: mlo wa asubuhi, wa mchana na wa jioni, kwa kuzingatia mahitaji ya mama mjamzito, mtoto chini ya miaka mitano, na mtu mzima wa kawaida.

Lengo kuu la mashindano haya ni kubuni mapishi mapya na ya ubunifu ya mazao hayo, ambayo yataongezwa kwenye mapishi ya kawaida tuliyozoea. Kupitia mashindano haya, inatarajiwa kuhamasisha jamii kuhusu faida za ulaji wa mazao haya yenye virutubisho muhimu kwa afya ya binadamu.

Kwa muda mrefu, wananchi wengi wamekuwa wakidhania kuwa mazao kama dengu, choroko na mbaazi ni ya kuuzwa nje ya nchi pekee, bila kutambua kuwa ni mazao ya asili yenye thamani kubwa ya lishe. Mashindano haya yanatoa hamasa mpya ya kuyatambua kama sehemu muhimu ya mlo wa familia.

Mashindano haya yanahusisha timu tatu, ambazo ni timu ya mapishi ya dengu, timu ya mapishi ya choroko, na timu ya mapishi ya mbaazi. Jumla ya washiriki ni 24, ambapo kila timu ina washiriki wanane (8) waliotoka katika mikoa ya Tanga, Mwanza, Singida, Manyara, Arusha na Kilimanjaro.

Baadhi ya wananchi waliopata fursa ya kuonja vyakula vilivyopikwa na wabunifu hao wameeleza kufurahishwa na ubunifu huo. Bi Rayana Alphonce, mkazi wa Tanga, amesema:

“Tumezoea kula wali na ugali, kumbe tunaweza kubadilisha mlo wa familia kwa kuandaa vyakula vitokanavyo na mazao haya. Vyakula hivi vimenivutia sana.”

Kauli kama hiyo pia zimetolewa na Bi Farida Ilali Hemed wa Barabara ya 16 na Bi Rehema Alphonce Mzule wa Barabara ya 20, jijini Tanga. 

Wananchi hao wamesema mashindano haya yamewafungua macho kuona uwezekano wa kutumia mazao ya ndani katika kuandaa mlo bora wa familia.

Maandalizi na ubunifu wa mapishi hayo yataendelea kwa siku chache zijazo, huku wapishi kutoka mikoa mbalimbali wakiendelea kuonyesha vipaji vyao katika kuandaa milo yenye ubunifu na lishe bora. 


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464