Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Patrobas Katambi, amekutana na makundi mbalimbali yakiwamo ya Bodaboda, Bajaji, Mama Lishe, Fundi Cherehani na Wafanyabiashara, kwa lengo la kuwahamasisha wajitokeze kwa wingi kwenye mkutano wa Mgombea Urais wa CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, utakaofanyika kesho katika Uwanja wa CCM Kambarage.
Katambi amezungumza na makundi hayo leo Oktoba 10, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa CCM Mkoa wa Shinyanga, ambapo amewasisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kumpokea na kumsikiliza Rais Samia.
Amesema Rais Samia ni kiongozi mwenye moyo wa kujali wananchi wote, pamoja na makundi ya wajasiriamali wadogo, kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji kiuchumi na mikopo nafuu, hivyo ni muhimu wakajitokeza kumpa sapoti na kumsikiliza hotuba yake kesho.
“Kesho ni siku ya kihistoria hapa Shinyanga, Jitokezeni kwa wingi mje mmsikilize Mgombea wetu wa Urais kupitia CCM Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, katika Uwanja wa CCM Kambarage, msikilize sera na Ilani ya CCM, nini ambacho amekifanya katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, na atafanya nini katika miaka mitano ijayo,”amesema Katambi.
Ameongeza kuwa, baada ya kujitokeza kumpokea Rais hapo kesho,wajitokeze tena kwa wingi Oktoba 29, 2025, kwenda kupiga kura za ushindi kwa Rais Samia, Wabunge na Madiwani wote wa CCM.
Aidha,Katambi ameeleza kuwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia, miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa katika Jimbo la Shinyanga Mjini, ikiwamo Ujenzi wa Uwanja wa Ndege, kukamilika kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, na sasa anajenga tena Stendi Kuu ya Mabasi pamoja na barabara ya lami inayoelekea hospitali ya Mkoa.
Amesema katika miaka mingine mitano ijayo,serikali ya CCM italeta kimbunga cha maendeleo Shinyanga Mjini, na kwamba yeye ni kiongozi mwenye kujali maslahi ya wananchi wake, na ndiyo maana hata fedha za mfuko wa jimbo hua anazisema hadharani na hakuna hata senti moja inayopotea.
Katambi pia amewahakikishia wajasiriamali hao kuwa wataendelea kunufaika na fursa za mikopo ya uwezeshaji pamoja na kuboreshewa mazingira ya kufanyia biashara, ikiwemo ujenzi wa masoko na miundombinu ya barabara.
Uchaguzi Mkuu wa Tanzania unatanyika Oktoba 29,2025, ambapo wananchi watapiga kura kuchagua Madiwani, Wabunge na Rais, ambapo kwa sasa, wagombea kutoka vyama mbalimbali wanaendelea kunadi sera na Ilani zao kwa wananchi kote nchini.
TAZAMA PICHA👇👇
Mgombea Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia CCM Patrobas Katambi akizungumza na makundi mbalimbali.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia CCM Patrobas Katambi akiwa juu ya Farasi kuhamasisha wananchi ujio wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kesho CCM Kambarage.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464










