Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),Patrobas Katambi, ameendelea na mikutano yake ya kampeni kwa kunadi sera na Ilani ya CCM, akiwataka wananchi wamchague kuwa Mbunge wao Oktoba 29, pamoja na kumpigia kura nyingi za ushindi Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na wagombea wote wa udiwani wa chama hicho.
Katambi leo Oktoba 8,2025 amefanya Mkutano mkubwa wa Kampeni kwa kuzungumza na wananchi wa Kata ya Kambarage,mkutano ambao umehudhuriwa na mamia ya wananchi wa Kata hiyo.
Akizungumza kwenye mkutano huo amesema yeye ni Mbunge wa maendeleo, huku akimshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, kwamba kila kitu ambacho hua anamuomba humpatia, na katika Kata hiyo ya Kambarage ameahidi wanakwenda kujenga soko kubwa la kisasa,na kuboresha mazingira rafiki ya wafanyabiashara.
“Niliwaambia kipindi naomba kura mwaka 2020 mimi ni Mbunge wa maendeleo,leo hii mmeona shughuli yangu kila kona yapo maendeleo, na ninajua kutafuta pesa za maendeleo kona zote za Bungeni nazijua, na uzuri Mama kila ninacho muomba hua ananipa, na sasa mnaona Shinyanga ilivyobadilika,”amesema Katambi.
Amesema, mfano hapo Kambarange wameboresha Kituo cha Afya,kuweka vifaa tiba vya kisasa ikiwamo X-RAY,upatikanaji wa Madawa,Madaktari, na wameboresha pia Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga na Rufaa ya Mkoa, pamoja na kuongeza magari ya kubeba wagonjwa “Ambulance”.
Ameongeza katika Sekta hiyo ya Afya wamejenga Vituo vya Afya na Zahanati mpya, na kwamba wamejenga barabara ya kiwango cha Lami kwenye Kituo cha Afya Kambarage, na pia wanajenga Lami ya kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Aidha,amesema kwa upande wa ujenzi wa miundombinu pia wanajenga Stand Kubwa ya kisasa ya Mkoa,Uwanjwa Ndege Ibadakuli,huku sekta ya elimu wamejenga shule mpya 10 na kuboresha miundombinu yote ya elimu ikiwako ujenzi vyumba vya madarasa na upatikanaji wa vyuo vikuu.
“Nawaombeni sana wananchi wa Kambarage siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mjitokeze kwa wingi kunipigia kura,Rais wetu Samia Suluhu Hassan, na Madiwani wote wa CCM akiwamo wa hapa Kambarage Khamis Haji ili tuwaletee maendeleo zaidi,”amesema Katambi.
Naye Mjumbe wa Kamati ya siasa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Mhandisi James Jumbe,akizungumza kwenye mkutano huo wa kampeni,amemombea kura nyingi za ushindi Patrobas Katambi,ili Rais Samia aendelee kumwamini na kumpatia nafasi ya kuendelea kuwa Naibu Waziri na hata kumpatia Uwaziri, ili awatumikie wananchi wa Shinyanga na kuwaletea maendeleo.
Amesema yeye alikuwa ni miongoni mwa watia nia kugombea nafasi ya Ubunge katika Jimbo hilo, lakini jina lake halikurudi, na kwamba baada ya hapo wapinzani wamlipigia simu hadi ngazi za kitaifa ili ahamie upande wa pili,lakini aligoma sababu yeye ni mwana CCM, na anamuunga mkono Patrobas Katambi na watashirikiana naye kwenye maendeleo.
“Ndugu zangu mliokuwa na maumivu baada ya jina langu kutorudi na mliokuwa na mashaka na mimi, sasa acheni,mimi ni mwana CCM na Moyo wangu nimeufungua, na Katambi ni kiongozi mzuri ana uzoefu na ameleta maendeleo, na waomba mpigieni kura nyingi za ushindi ili Rais Samia aendelee kumwamini na kumpatia nafasi ya Uwaziri,Mbunge akiwa Waziri hua kunafaida nyingi,”amesema Jumbe.
Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Anold Makombe,amewataka wananchi wa Kambarage na Jimbo zima la Shinyanga Mjini, kwamba Oktoba 29 wasifanye makosa, bali wakatiki kwa wagombea wote wa CCM, kuanzia nafasi ya Udiwani,Mbunge Katambi na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
TAZAMA PICHA👇👇
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia CCM Patrobas Katambi akinadi sera la ilani ya CCM kwa wananchi wa Kambarage katika mkutano wa kampeni.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia CCM Patrobas Katambi (kulia)akimnadi Mgombea Udiwani wa Kata ya Kambarage Khamis Haji.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Anold Makombe akizungumza kwenye mkutano huo wa kampeni.
Mjumbe wa Kamati ya siasa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Mhandisi James Jumbe akizungumza kwenye mkutano huo wa kampeni.