` WANAWAKE 81 WAHITIMU MAFUNZO YA UFUNDI VETA SHINYANGA KUPITIA PROGRAMU YA WANAWAKE NA SAMIA

WANAWAKE 81 WAHITIMU MAFUNZO YA UFUNDI VETA SHINYANGA KUPITIA PROGRAMU YA WANAWAKE NA SAMIA

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

WANAWAKE 81 wamehitimu mafunzo ya ufundi bure katika fani mbalimbali kupitia Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mkoani Shinyanga, chini ya programu ya Wanawake na Samia.

Mahafali hayo yamefanyika leo Oktoba 2,2025, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita.
Akizungumza katika mahafali hayo,Mhita amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha programu hiyo inayowawezesha wanawake kupata ujuzi wa ufundi na kujikwamua kiuchumi.

“Mafunzo haya yamewajengea uwezo wa kujiajiri na kuimarisha uchumi wa familia zao,” amesema Mhita.
Aidha, ametoa wito kwa wahitimu hao kuunda vikundi vya ujasiriamali ili waweze kupata mikopo ya Halmashauri isiyo na riba inayotolewa kwa asilimia 10, ambapo wanawake hunufaika kwa asilimia nne,huku akiwasihi kuchangamkia mikopo ya taasisi nyingine za kifedha.

Ameongeza kuwa, serikali itaendelea kuwapatia fursa za mikopo na miradi kupitia Halmashauri, huku akiwaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii kuwapatia wahitimu hao elimu ya namna ya kuzitumia fursa hizo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Samia Taifa Futuma Madidi, amemshukuru Rais Samia kwa kuanzisha programu hiyo iliyowawezesha wanawake wengi kupata ujuzi wa ufundi,huku akitoa wito kwa serikali kuwapatia wahitimu hao vipaumbele kwenye zabuni na fursa nyingine za kiuchumi.

Naye Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga Abraham Mbughuni,ametaja fani walizosomea wanawake hao na idadi yao kuwa saluni (25), mapambo (4), umeme (10), kompyuta (2), bomba (7), udereva (4), ushonaji (26) na mapishi (3), na kufanya jumla ya wahitimu kufikia 81.
Baadhi ya wahitimu akiwamo Zainabu Joseph, wamemshukuru Rais Samia kwa kuanzisha programu hiyo, wakisema imewapatia ujuzi wa kuendesha maisha na kujipatia kipato.

TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza kwenye mafahali ya wahitimu wa program ya wanawake na Samia.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Samia Taifa Futuma Madidi akizungumza.
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Magharibi Asanterabi Kanza akizungumza kwenye mahafali.
Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga Abraham Mbughuni akisoma taarifa ya mafunzo hayo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464