Na MWANDISHI WETU, Geita
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ametembelea banda la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika Maonesho ya Nane ya Madini yanayoendelea kwenye Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mkoani Geita, na kuipongeza NSSF kwa huduma zake za kidijitali kwa wananchi na wadau.
Akiwa kwenye banda hilo tarehe 22 Septemba 2025, Mhe. Waziri Mkuu alipokea maelezo kutoka kwa Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Bi. Lulu Mengele, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Masha Mshomba, kuhusu jitihada za Mfuko kutekeleza maelekezo ya Serikali ikiwemo kuhakikisha elimu ya hifadhi ya jamii inaendelea kutolewa kwa sekta binafsi na wananchi waliojiajiri.
Bi. Lulu alisema: “Mafanikio yetu makubwa yametokana na mwongozo wa Serikali wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, rahisi na kwa wakati kupitia mifumo ya kidijitali.”
Aidha, alimwonesha Waziri Mkuu mifumo ya kidijitali inayorahisisha upatikanaji wa huduma zote kwa mwanachama, ikiwemo huduma zinazopatikana kupitia simu za kiganjani, iwe ni simu janja au ya kawaida, ambapo wote wanahudumiwa na NSSF kidijitali.
“Wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia madarakani, thamani ya Mfuko ilikuwa shilingi trilioni 4.8, na sasa imefikia trilioni 9.9,” alisema Bi. Lulu.
Kwa upande wake, Meneja wa NSSF Mkoa wa Geita, Bi. Winniel Lusingu, aliwataka wananchi kutembelea banda la NSSF ili kupata elimu ya hifadhi ya jamii.