Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga na mgeni rasmi wa maadhimisho ya siku ya Usafishaji Duniani ngazi ya Wilaya Mhe.Peter N. Masindi akizungumza na Wananchi wa Wilaya hiyo namha ya kuhifadhi taka wakati wa zoezi la ufanyaji usafi maeneo mbalimbali yanayotoa huduma za kijamii Septemba 20,2025
Na Sumia Salum – Kishapu
Wakati Dunia ikiadhimisha Siku ya Usafishaji Mazingira, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi, ametoa onyo kali kwa wote wasiothamini usafi na wanaoharibu mazingira, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Akizungumza Septemba 20, 2025, kwenye maadhimisho ya siku hiyo ngazi ya Wilaya akiwa ndiye Mgeni rasmi, Mhe. Masindi amesema wananchi wote wana wajibu wa kutunza mazingira yanayowazunguka hususani yale yanayotoa huduma za jamii ikiwemo vituo vya mabasi, hospitali, masoko, magulio, mitaro na pembezeni mwa barabara.
“Ni marufuku kuchoma moto taka kwenye mazingira ya makazi. Hakikisheni mnatunza taka na kuzipeleka dampo la muda la Shireku. Taka zinazooza mnaweza kuzichimbia kwenye mashimo kisha kutumia mboji yake kuongeza rutuba mashambani,” amesema Masindi.

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga na mgeni rasmi wa maadhimisho ya siku ya Usafishaji Duniani ngazi ya Wilaya Mhe.Peter N. Masindi akizungumza na Wananchi wa Wilaya hiyo baada ya zoezi la ufanyaji usafi maeneo mbalimbali yanayotoa huduma za kijamii Septemba 20,2025
Amesema suala la usafi ni la lazima na sio ombi, na kumuelekeza Afisa Mazingira wa Wilaya kuhakikisha vifaa vya kuhifadhia taka vinaongezwa maeneo ya barabarani, vituo vya mabasi na kuimarisha elimu ya uhifadhi wa mazingira.
“Asiwepo wa kuufanya mji wetu wa Kishapu kuwa mchafu. Mifuko ya plastiki ni marufuku. Ni kosa pia kutupa chupa au vifungashio vya vinywaji mitaani na mitaroni. Atakayebainika, sheria itachukua mkondo wake,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Mhe. Masindi amewataka wananchi kuendelea kujenga vyoo bora na vya kisasa ili kulinda afya na kupunguza uchafuzi wa mazingira, hasa kwenye vyanzo vya maji.
" Ninyi mnaosubiria watu wamelala mnaenda kutupa taka maeneo yasiyorasmi nawatumia salam serikali Iko kazini na ninyi wenye tabia ya kujisaidia na Kuhifadhia kinyesi kwenye mifuko kisha kuitupa kwenye vyanzo vya Maji ukibainika Sheria haitakuvumilia uchafu umepelekea watu wengi tuliowapenda na kutamani tuwe nao Leo hawapo Tena kwani magonjwa yasababishwayo na uchafu ikiwemo Kipindupindu yaliwaondolea uhai hivyo hatutaruhusu tena uzembe kwenye uhai wa watu" ameongeza Mkuu huyo Wilaya
Masindi ametoa wito kwa wananchi kila kaya kupanda miti ifikapo msimu wa mvua mwezi Novemba, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Vilevile, amehimiza wananchi kushiriki kikamilifu uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 kwa amani, kwa kuchagua viongozi wenye maono ya kutatua kero za wananchi.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu, Bi. Fatma H. Mohamed, amewapongeza wananchi waliojitokeza kushiriki zoezi la usafi, akisema wameonesha mshikamano wa dhati kwa serikali.
Afisa Mazingira wa Wilaya hiyo, Cassim Salim Said, amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa usafi na kuonesha kwamba taka zina thamani endapo zitachakatwa kwa njia sahihi.
“Sasa hivi tuko kwenye dunia yenye teknolojia; kila taka inafaida. Tunahakikisha wananchi wanapata elimu ya usafi na thamani ya taka, hata wanafunzi mashuleni,” amesema Said.

Baadhi ya wakazi wa Mhunze, Josephina Methew na Cesilia Jackson, wameeleza kuwa maadhimisho hayo yamekuwa kumbusho muhimu kwa jamii kuhusu wajibu wa kutunza mazingira, kwani afya bora inategemea mazingira safi.
Ikumbukwe kuwa Septemba 10, 2025, TFS Kishapu kupitia Mhifadhi Misitu wa Wilaya, Tumaini Masatu Mwijarubi, ilitangaza mpango wa kuotesha miche 200,000 ya matunda, mbao na kivuli kwa wananchi bure ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi kuelekea msimu wa mvua hapo baadae.
Usafi wa pamoja umefanyika maeneo mbalimbali ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mhunze, ukihusisha pia wadau wa Shirika la TCRS. Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo: “Tunza Mazingira kwa Kuzipa Taka Thamani".





































































Watumishi kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga baada ya zoezi la Usafi



Muonekano wa Dampo la muda lililotengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga lililoko Shireku wakati maandalizi ya ujenzi wa Dampo la kisasa yakiendelea litakalokuwa maeneo ya SulagiWilayani humo