
Na Eunice Kanumba-Shinyanga
Kampuni ya Jambo Group ya mjini Shinyanga sasa ni mdhamini mkuu wa timu ya Pamba FC ya jijini Mwanza katika msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kuanza rasmi Septemba 16, 2025. Makubaliano ya udhamini huo yamesainiwa leo katika ofisi za kampuni hiyo zilizopo Kata ya Ibadakuli, Manispaa ya Shinyanga.
Akizungumza hayo leo Septemba 13 ,kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jambo Group, Meneja wa Jambo Media na msimamizi wa chapa, Nickson George, alisema hatua hiyo siyo tu udhamini, bali ni ushirikiano wa kibiashara na kijamii utakaosaidia kukuza chapa za pande zote mbili kupitia michezo.
“Leo ni historia ya azimio la pamoja kati ya taasisi yetu na uongozi wa Pamba FC. Mkataba huu una lengo kuu la kukuza chapa zote mbili, hususan bidhaa za Jambo Group,” alisema George.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Pamba FC, Peter Lehlet, alisema udhamini huo ni mwanzo wa ukurasa mpya wa mafanikio kwa klabu hiyo. Alifafanua kuwa Pamba na Jambo Group walishirikiana awali, wakasitisha kwa muda, lakini sasa wamerejea tena kuendeleza gurudumu la michezo.

Kwa upande wa wachezaji, Nahodha wa timu hiyo, James Mwashinga, aliahidi kupambana na kufanya vizuri katika msimu huu ili kuipa heshima chapa ya Jambo Group na mashabiki wa Pamba FC.
Pamba FC inatarajiwa kushuka dimbani Septemba 18, 2025 dhidi ya Namungo FC katika Uwanja wa Majaliwa, mkoani Lindi, ikiwa ni mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu.
Kampuni ya Jambo Group imekuwa mdau mkubwa wa soka nchini kwa nyakati tofauti, ikiwahi kudhamini timu mbalimbali za ukanda wa ziwa, ikiwemo Stand United ya Shinyanga.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464