
Na Kareny Masasy, Ushetu
MGOMBEA Ubunge kupitia chama cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Ushetu Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga Emanuel Cherehani amesema wananchi waendelee kumuamini na kumchagua ili aweze kukamilisha miradi iliyotengewa fedha na serikali ambayo inaendelea kutekelezwa na kuendelea kutatua changamoto zingine ikiwemo suala la kilimo.
Pia amesema Serikali imetoa shilingi Bilioni
156 kwa jimbo hilo kwaajili ya shughuli za Maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyumba vya
madarasa, miundombinu ya barabara na kuweka nishati ya Umeme ambavyo vyote amevipigania na fedha kupatikana.
Cherehani
amesema hayo tarehe 13.Septemba,2025
kwenye uzinduzi wa Kampeni wa jimbo hilo uliofanyika kijiji cha
Iramba kata ya Igwamanoni ambapo alieleza jimbo hilo lina kata 20,vijiji
122 na vitongoji 550 ikiwa aliingia madarakani mwaka 2021 mwezi Oktoba
baada ya mbunge aliyekuwepo kufariki alikuta vijiji 70 tu ndiyo vina
nishati ya Umeme.
Cherehani amesema serikali ilileta
shilingi Bilioni 156 kwa nyakati tofauti kwaajili ya kutatua kero za
wananchi kwani kuna mradi wa sola unaogharimu shilingi Bilioni 11.7
unaoendelea kujengwa kijiji cha Kayenze na wakandarasi bado wanaendelea
na kazi na tayari kuna sola zaidi ya 200 zipo tayari.
"Mpaka sasa vijiji vyote 112 vina nishati ya umeme na baadhi
ya vitongoji hivyo tupeni kura chama cha Mapinduzi wagombea wote wa Udiwani,
Ubunge na Rais tutekeleze yale ambayo tumeanza nayo na
kuyakamilisha na lengo la kuwa na mradi mkubwa wa Sola
tunataka kila kitongoji kuwe na umeme kuongeza nguvu ya umeme uwe wa
uhakika maeneo yote."amesema Cherehani.
Cherehani amesema zaidi ya shilingi Bilioni 9.2 zimeletwa na serikali
jimboni hapo na kujenga vyumba vya madarasa 230 na shilingi Milion
540 zimejenga shule ya sekondari Mweri ya wasichana na hakuna mwananchi
aliyechangishwa fedha zake na watoto wanasoma vizuri.
Cherehani amesema bado kuna changamoto
ya miundombinu ya barabara kuwa mibovu ambapo jimbo hilo walipata shilingi
Milioni 600 kwaajili kuweka Molamu baadhi ya barabara na endapo wananchi
wakimpatia ridhaa ya kuongoza tena atahakikisha barabara za kuunganisha
kutoka kijiji kimoja kwenda kingine zinaboreshwa zaidi na kupitika kirahisi.
Mgombea diwani wa kata ya Igwamanoni Gagi Lala amesema vijiji vyote
saba vina nishati ya umeme,kuna zahanati mbili na kituo cha afya
kimoja, lakini zahanati zingine zinajengwa mbili nakufikisha hospitali
tano ndani ya kata moja , maji ya kisima kirefu ndiyo wanatumia ni kazi
ya Chama Cha Mapinduzi ambayo imetekeleza ilani yake na itaendelea
kutekeleza wakiichagua.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa amesema
ilani ya chama imeeleza vizuri kila
changamoto inakwenda kutekelezwa hivyo wachague chama hicho na wagombea wake
kwani ilani itatekelezwa kwa kuwachagua wote wanaotokana na chama hicho na
mambo makubwa yamefanyika yanaonekana ndani ya mkoa huu ikiwemo Ruzuku ya
mbolea kwa wakulima.

Mkazi wa kata ya Nyamilangano Sawaka Sagenge amesema wanachotaka viongozi watakao chaguliwa mwaka
huu wahakikishe changamoto zinaenda kutatuliwa kwani
wanahitaji barabara yenye urefu wa kilomita 54 iwe ya lami
inayotoka kwenye kata hiyo hadi mjini Kahama kwani ina kiwango cha changarawe
ambayo ndiyo kiungo kikuu kwenye jimbo hili.
Mkazi wa Kitongoji cha kipangu kata Igwamanoni Gaudensia Mahushi
amesema viongozi watakao wachagua
wanaomba nishati ya umeme kwenye kitongoji hicho kwani umeme umeishia
kwenye kijiji pekee na miundombinu ya barabara mibovu wakitaka kwenda
kijiji jirani wanazunguka hakuna barabara kabisa hata wakiwa wanakwenda kwenye
Zahanati ni changamoto.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464