
Mwenyekiti wa kamati ya dini mbalimbali mkoa wa Shinyanga Sheikh Soud Kategile.

NA EUNICE KANUMBA - SHINYANGA
Jumuia ya Kikristo Tanzania (CCT) leo tarehe 8 Septemba mwaka 2025 imeendesha Semina kuhusiana na elimu ya uraia na uchaguzi kwa viongozi wa dini, kupitia kamati ya dini mbalimbali ya mkoani Shinyanga lengo likiwa ni kuimarisha mahusiano mema miongoni mwa waumini wa dini hizo pamoja na kulinda amani na utulivu kwa taifa la Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari mratibu wa dawati la mahusiano ya dini mbalimbali kutoka jumuia ya kikristo Tanzania (CCT) mchungaji David Kalinga amesema Jumuiya hiyo imeendesha semina hiyo mahususi katika kipindi hiki cha uchaguzi kwani viongozi hao wana wafuasi katika nyumba zao za ibada hivyo dhima kubwa waliyonayo ni kuwaelimisha juu ya wajibu wao wa msingi wa kupiga na kupigiwa kura ili nao wakawaelimishe waumini katika nyumba zao za ibada.
“Tumefanikiwa kuwepo Shinyanga na kuzungumza na Kamati ya dini mbalimbali kwa kuwakusanya viongozi wa kikiristo na kiislamu kwa lengo la kuendelea kuimarisha mahusiano mema pia kutoa elimu ya uraia na uchaguzi”, amesema mchungaji David Kalinga.
Kwa upande wake mwezeshaji wa semina hiyo katika masuala ya sheria za uchaguzi mwanasheria Judith Mwasambili amesema wameamua kutoa elimu ya sheria za uchaguzi kwa viongozi hao ili nao waweze kuifikisha kwa waumini wa dini zao hali itakayopelekea kila mtu kuzifahamu sheria za uchaguzi na kujitokeza kupiga kura tarehe 29 Oktoba 2025.
Naye mwenyekiti wa kamati ya dini mbalimbali mkoa wa Shinyanga Sheikh Soud Kategile amesema elimu hiyo waliyoipata wataifikisha kwa waumini ambapo pia ametoa rai kwa wananchi kujitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi huku akiviomba vyombo vya dola kusimamia masuala yote ya uchaguzi kwa haki psipo kupendelea chama chochote cha siasa lakini pia amevitaka vyama vya siasa kufanya kampeni za kistaarabu pasipo kutoa lugha za kuudhi kwa wengine.
Mwinjilisti wa kanisa la AICT Evelyn Pole amesema kuwa kupitia elimu waliyopata watakwenda kuwaelekeza washirika wao juu ya umuhimu na namna ya kwenda kupiga kura na kuwajulisha kuwa ni haki yao kwa mujibu kwa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha Sheikh wa kata ya mjini Majaliwa Masoud amesema wao kama viongozi wa dini wana haki ya kwenda kuwaelimisha waumini wao juu ya haki na wajibu wao katika suala zima la upigaji kura huku akiitaka jumuia hiyo ya kikiristo Tanzania (CCT) kuendelea kutoa elimu.
Nao baadhi ya viongozi wa dini waliohudhuria semina hiyo akiwemo mchungaji Mathias Chidama ambaye pia ni katibu wa jumuia ya kikiristo Tanzania (CCT) mkoa wa Shinyanga amesema kuwa watakwenda kufikisha elimu hiyo waliyopatiwa kwa waumini na kuwahamsisha kujitokeza kupiga kura.


Sheikh Majaliwa Masoud
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464