KATAMBI BABALAO,ATIKISA UZINDUZI WA KAMPENI ZA CCM JIMBO LA SHINYANGA MJINI
Odilia Batimayo CCM ikiahidi inatekeleza
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga Odilia Batimayo,amezindua rasmi Kampeni za CCM Jimbo la Shinyanga Mjini,huku akimwagia sifa Mgombea Ubunge wa Jimbo hilo kupitia (CCM) Patrobas Katambi,kuwa ni kijana ambaye hana Mbambamba, bali yeye ni mtu wa kazi tu na kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Uzinduzi huo umefanyika leo Septemba 14,2025 katika Kata ya Ndala na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi,wana CCM pamoja na Wagombea Udiwani Kata zote 17 za Shinyanga Mjini.
Odilia akizungumza kwenye kampeni hizo,amesema Katambi ni kijana mdogo lakini mambo yake ni makubwa, ambapo ndani ya miaka mitano amelitendea haki Jimbo la Shinyanga kwa kutekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo na kuwaletea maendeleo wananchi.
“CCM ikiahidi inatekeleza,hivyo nawaomba wananchi endeleeni kukiamini Chama Cha Mapinduzi na siku ya Uchaguzi Oktoba 29,mpigieni kura za ndiyo Mgombea Urais,Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,Patrobas Katambi na Wagombea udiwani wote wanaotokana na CCM,”amesema Odilia.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Anold Makombe, akizungumza kwenye uzinduzi huo wa kampeni amemuombea kura Mgombea Urais wa CCM,Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, Patrobas Katambi na Madiwani wote wa CCM kuwa wao ndiyo watawaletea maendeleo ya kweli na siyo vyama vingine.
Naye Mgombea Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi,amewaeleza wananchi wa Ndala baadhi ya maendeleo ambayo ameyafanya katika Jimbo hilo ndani ya miaka mitano, kuwa katika sekta ya elimu wamejenga shule mpya 10,Tano za Shule ya Msingi na Tano Sekondari, pamoja na kupanua Chuo Cha Ushirika Moshi Tawi la Shinyanga, Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto, kuleta Chuo cha Madini pamoja na Cha Serikali za Mitaa Hombolo.
Kwa Upande wa Sekta ya Afya, kuwa wamejenga Zahanati mpya 9,Vituo vya Afya kikiwamo cha Ihapa,kuboresha Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga na kukamilisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na sasa inatoa huduma za matibabu kwa wananchi.
Amezungumzia pia suala la miundombinu, kuwa wamejenga Madaraja ambayo yalikuwa Korofi,Makarati,Vivuko,ujenzi wa masoko, upanuzi uwanja wa ndege Ibadakuli, na sasa wapo kwenye ujenzi wa Stand Mpya ya Kisasa eneo la Kizumbi,na Barabara ya Lami kwenye Hospitali ya Mkoa Mwawaza.
Amezunguzia pia suala la Maji kwamba takribani maeneo yote ya Shinyanga yanapata huduma ya majisafi na salama, huku akigusia suala la umeme kwamba kati ya vijijini 17 vya manispaa ya Shinyanga vijiji 7 ndiyo vimebaki kupata umeme.

Aidha,amesema endapo akipata ridhaa ya wananchi wa Shinyanga kuchagua tena kuwa Mbunge wao Oktoba 29,na kumchagua Rais Samia na Madiwani wote wa CCM kwamba mvua ya maendeleo itaendelea kumiminika jimbo humo, sababu kwenye ilani ya CCM (2025-2030)imebainisha miradi mingi ya maendeleo ambayo inapaswa kutekeleza kwa wananchi.
Oktoba 29 ni Uchaguzi Mkuu wa kuchagua Madiwani,Wabunge na Rais.
TAZAMA PICHA👇👇
Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga Odilia Batimayo akizungumza kwenye uzinduzi wa Kampeni za CCM Jimbo la Shinyanga Mjini.
Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga Odilia Batimayo akimnadi Mgombea Ubunge wa CCM Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi (kulia).
Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga Odilia Batimayo akiomba kura za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,Patrobas Katambi na Madiwani wote wa CCM.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Anold Makombe akizungumza kwenye uzinduzi wa Kampeni.
Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Hamisa Chacha akizungumza kwenye uzinduzi wa Kampeni.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia CCM Patrobas Katambi akinadi sera kwa wananchi wa Ndala wakati wa uzinduzi wa Kampeni.

