Na Marco Maduhu,SHINYANGA
Kampuni ya Jambo Group,imesema itaacha kuifadhili Timu ya Stand United,kama haitapata ushirikiano kutoka kwa wadau wengine wa michezo mkoani Shinyanga,kuungana pamoja kui "support" timu hiyo.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 10,2025 na Mratibu wa Masuala ya michezo katika Timu ambazo zinafadhiliwa na kiwanda cha Jambo Crispine Kakwaya,wakati akizungumza na waandishi wa habari kufuatia hali ya Timu hiyo.
Crispine Kakwaya.
Amesema Timu ya Stand United siyo ya Jambo Group, bali ni timu ya wanashinyanga wote kwa ujumla,na wao walikuwa wafadhili tu, hivyo ni jukumu la kila mwana shinyanga kuichangia timu yao,na kuunganisha nguvu kuisaidia timu yao ili ifanye vizuri.
“Tume waita hapa waandishi wa habari, ili kuweka mambo sawa kutokana na maswali ambayo mmekuwa mkituuliza Jambo Group kutokana na ukimya uliopo juu ya Stand United,kwanza watu wanapaswa kujua kwamba Stand United siyo timu ya Jambo ni Timu ya wanashinyanga wote kwa ujumla,”anasema Kakwaya na kuongeza.
”Sisi Jambo Group tulikuwa tunahitaji ushirikiano kutoka kwa watu tofauti tofauti ili kuunganisha nguvu,ushirikiano ambao umeonekana kuwa Changamoto kupatikana kama msimu uliopita, hivyo tukaamua kukaa kimya kusubili ushirikiano huo ambao hadi sasa tumeona hakuna kinachoendelea”.
Aidha,amesema endapo kama watu au wadau wa michezo wakaendelea kukaa kimya na kujiweka pembeni juu ya kuisupport timu hiyo, basi na wao Jambo Group watajiweka pembeni,maana wao peke yao hawatoshi kuisupport timu hiyo.
Amesema,wao kama Jambo Group wapo tayari kushirikiana na wadau wengine kuisaidia Timu ya Stand United ili kufikia malengo ya kupanda Ligi kuu, lakini wao peke yao hawezi sababu Timu hiyo siyo ya Jambo,na kwamba kazi ya kuendesha timu ni gharama kubwa, hivyo nguvu ya mtu mmoja haitoshi kufikia malengo ya taasisi.
“Mimi msimu uliopita bahati nzuri nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya usajili na Mashindano Timu ya Stand United, kazi niliona ilivyokuwa ngumu ambapo nguvu ya mtu mmoja haitoshi kufikia malengo ya taasisi flani, na ndiyo maana Timu nyingi zinazofanikiwa zina mjumuiko wa nguvu kutoka maeneo tofauti tofauti, na hapa kwetu Shinyanga kuna wafanyabiashara wengi, Makampuni mengi ya vinywaji, na Migodi mingi ya Madini, ambapo wanahitaji kuungana na kusaidia Timu,”amesema Kakwaya.
Katika hatua nyingine, amesema hawajakata tamaa na timu hiyo sababu, wao hua wanarudisha kwa jamii na Timu ya Stand United ipo hapo Shinyang, na hawapendi kuona timu ikidondoka, bali wanahitaji support kutoka kwa wadau wengine ili kuongeza nguvu, na kusisitiza kwamba wasipoona support yoyote kutoka kwa wadau au serikali,basi na wao watajiweka kando.
“Tunaomba ushirikiano,kama huo ushirikiano hautokuwepo, maana yake na sisi tunaona kuwa jamii hii kitu haikitaki, hivyo tutakaa pembeni,”amesisitiza Kakwaya.
Nao baadhi ya Mashabiki wa Timu ya Stand United, wameiomba serikali iingilie kati kuisupport timu yao,ili ifanye vizuri katika ligi ya Championship na kupanda hadi Ligi Kuu, na kuleta furaha kwa wananchi wa Shinyanga n ahata kuchochea ukuaji wa uchumi pale Timu zitakapokuwa zikija kucheza Shinyanga.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464




