Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MGOMBEA wa nafasi ya udiwani Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga,kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM)Pendo John Sawa, ameizindua rasmi kampeni ya kunadi sera na kuomba kura kwa wananchi,ili wamchague kuwa diwani wao katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29,2025.
Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika leo Septemba 8,2025 katika eneo la Butengwa,na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi, wanachama wa CCM,pamoja na wagombea udiwani kutoka kata jirani.
Akizungumza wakati akinadi sera zake,Pendo amewahidi wananchi wa kata hiyo kuzipatia ufumbuzi changamoto zao, ikiwamo ubovu wa barabara,ukosefu wa zahanati,na huduma ya umeme katika mitaa ambayo bado haina huduma hiyo.
Amesema pia ataanzisha mchakato wa kutafuta eneo la ujenzi wa shule mpya ya msingi, ili kuwapunguzia wanafunzi adha ya kuvuka barabara kubwa kwenda kusoma shule ya Mwalugoye.
“Oktoba 29 niadhimisheni imani kwa kunichagua, nawahakikishia wananchi wa Ndembezi sitaweza kuwaangusha, mnanifahamu kwa utendaji wangu kazi, na mimi huwa si shindwi” amesema Pendo.
Katika mkutano huo,wananchi pia wameombwa kumpigia kura za ushindi Rais Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi,ili CCM ishinde na kuendelee kuwaletea maendeleo Watanzania.
Kwa upande wake, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini Said Bwanga, ameasema Kata ya Ndembezi imepata mgombea mwenye uwezo mkubwa wa hoja na anayejituma, hivyo ataweza kuwawakilisha vyema halmashauri na kuwaletea maendeleo.
Oktoba 29,2025 ni siku ya kupiga kura kuchagua Madiwani,Wabunge na Rais,na sasa Wagombea wapo kwenye kampeni za kunadi sera za vyama vyao kwa wananchi.
TAZAMA PICHA👇👇
Mgombea Udiwani Kata ya Ndembezi Pendo John Sawa akinadi sera kwa wananchi.
Mwenzi wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Said Bwanga akimnadi kwa wananchi Mgombea Udiwani Kata ya Ndembezi Pendo John Sawa.
