Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akizungumza wakati akifunga mafunzo kwa waandishi wa habari na watangazaji kutoka Kanda ya Ziwa, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuhakikisha taarifa zinazohusu Uchaguzi Mkuu wa 2025 zinaripotiwa kwa weledi, usahihi na kwa kuzingatia maadili ya taaluma ya habari.
- Picha na Kadama Malunde
Na Marco Maduhu,MWANZA
MKUU wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda,amewataka waandishi wa habari nchini kuzingatia maadili na sheria wakati wa kuripoti taarifa za uchaguzi.
Amebainisha hayo leo Agosti 7,2025 wakati akifunga Semina ya Waandishi wa habari kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Jeshi la Polisi,katika kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.
Amesema vyombo vya habari vina deni kubwa kwa kuhakikisha uchaguzi Mkuu unafanyika kwa amani,kwa kuandika habari sahihi bila kuleta taharuki kwa jamii na kusababisha vurugu.
"Uchaguzi ni tukio nyeti hivyo ni vyema waandishi wa habari wakati wa kuripoti taarifa za uchaguzi ni vyema wakazingatia maadili na sheria ili kuandika habari kwa usahihi zisizoleta taharuki na machafuko,"amesema Mtanda.
Amewataka pia waandishi wa habari wajiepushe na Rushwa hasa kipindi cha Kampeni ili kutomchafua mgombea mwingine au kuficha taaarifa ambazo ni muhimu kwa jamii pamoja na kutoingia faragha za Wagombea.
Aidha,ametoa wito kwa Jeshi la Polisi kuwalinda Waandishi wahabari,wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ili wasiweze kupokea vitisho kutoka kwa baadhi ya Wagombea.
Katika hatua nyingine,amesema serikali itaendelea kulinda uhuru wa vyombo vya habari na kwamba alipoingia tu Madarakani Rais Samia Suluhu Hassan alivifungulia vyombo vya habari ambavyo vilikuwa vimefungiwa na kurekebisha baadhi ya sheria.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Rodney Mbuya,amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa waandishi wa habari pamoja na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha uchaguzi Mkuu wa 2025 unafanyika kwa amani na utulivu.
Katika semina hiyo,mada mbalimbali ziliwasilishwq ikiwamo Mwongozo wa Waaandishi wa habari, Wajibu wa Waandishi wa habari na Jeshi la Polisi, Maadili na Sheria za Waandishi wa habari, Matumizi ya akili Unde,Utangazaji na Migogoro,Majanga na ulinzi wa taarifa binafsi kuelekea uchaguzi mkuu.